Mamlaka za eneo la Gaza Jumanne jioni ziliishutumu Israel kwa kuiba viungo vya miili ya Wapalestina na kutaka uchunguzi wa kimataifa ufanyike.
Katika taarifa yake, ofisi ya vyombo vya habari vya serikali yenye makao yake makuu mjini Gaza imesema uchunguzi wa miili hiyo umebaini kuwa maumbo yao yalibadilika pakubwa kutokana na kuibwa kwa viungo muhimu vya maiti hizo.
Imeongeza kuwa jeshi la Israel lilikabidhi miili bila majina yao na kukataa kutaja ni wapi zilikamatwa. Pia imesema kuwa jeshi la Israel lilirudia kitendo hicho wakati wa vita vinavyoendelea Gaza na pia kufukua maiti kutoka makaburini.
Taarifa hiyo ilikosoa kile ilisema “msimamo wa kimya wa mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi huko Gaza, ikiwa ni pamoja na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, kuhusu uhalifu wa kutisha unaofanywa na (Israel).”
Mamlaka ya Israel bado haijatoa maoni yoyote kuhusu tuhuma hizo. Mapema siku ya Jumanne, mamlaka ya Israel ilitoa miili ya makumi ya Wapalestina waliouawa na jeshi la Israel ambao walikuwa wamezuiliwa wakati wa operesheni yake ya ardhini.