Mamlaka za afya huko Gaza zilisema kuwa vikosi vya Israeli viliizingira na kushambulia kwa makombora hospitali ya Indonesia katika mji wa Beit Lahia kaskazini mwa eneo hilo alfajiri ya Jumamosi, ripoti ya Agence France-Presse (AFP).
“Vifaru vya Israeli vimezunguka kabisa hospitali, kukata umeme na kupiga makombora hospitalini, ikilenga orofa ya pili na ya tatu kwa mizinga,” mkurugenzi wa kituo hicho, Marwan Sultan alisema. Aliongeza
Kuna hatari kubwa kwa wafanyikazi wa matibabu na wagonjwa.
Katika taarifa, wizara ya afya ya Gaza pia ilisema kuwa Israel ililenga orofa za juu, na kuongeza kuwa kulikuwa na “zaidi ya wagonjwa 40 na waliojeruhiwa pamoja na wafanyikazi wa matibabu” waliopo.
“Milio ya risasi nzito” kuelekea hospitali na ua wake ilizua “hali ya hofu kubwa” kati ya wagonjwa na wafanyikazi, iliongeza.
Israel ilianzisha mashambulizi mapya kaskazini mwa Gaza mapema mwezi huu, ikisema kuwa inalenga wapiganaji wa Hamas waliokuwa wanajipanga upya huko.
Shirika la ulinzi wa raia wa Gaza limesema shambulizi la Israel usiku wa kuamkia jana katika eneo la karibu la Jabalia liliua watu 33.
Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya kibinadamu siku ya Ijumaa liliendelea “kutoa tahadhari kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya na hatari ambayo raia wa kaskazini mwa Gaza wanakabiliwa nayo. Familia huko zinajaribu kuishi katika hali mbaya, chini ya mashambulizi makubwa ya mabomu.”