Manchester City imeishutumu Ligi Kuu ya Uingereza kwa kutoa taarifa za kupotosha baada ya kesi ya kisheria inayohusu kanuni za mikataba ya kibiashara. City iliandika barua kwa vilabu vingine 19 vya Ligi Kuu na uongozi wa ligi siku ya Jumatatu, ikipinga tafsiri ya ligi kuhusu uamuzi wa kesi hiyo. Klabu hiyo ilisema kuwa sheria zote zinazohusu mikataba na taasisi zinazohusiana na wamiliki wa vilabu (APT) sasa ni batili.
Sheria za APT ziliundwa ili kuhakikisha mikataba ya kibiashara kati ya vilabu na mashirika yanayohusiana na wamiliki wake inafanyika kwa thamani halisi ya soko, na si kwa makubaliano yaliyozidishwa. Hata hivyo, City ilifungua kesi mapema mwaka huu ikidai kuwa sheria hizo zinakiuka kanuni za ushindani. Ligi Kuu na Manchester City zote zilitangaza ushindi baada ya uamuzi wa jopo la usuluhishi kutolewa, ambapo ligi ilisema City haikufaulu katika mashtaka mengi waliyowasilisha.
Hata hivyo, City kupitia wakili wake mkuu, Simon Cliff, ilisema kuwa jopo hilo liliamua kuwa sheria za APT ni batili na kwamba Ligi Kuu imetumia vibaya nafasi yake ya nguvu sokoni. Pia alieleza kuwa ni jambo la kushangaza kwamba Ligi ilisema City haikushinda hoja nyingi walizowasilisha. Cliff alionya kuwa Ligi isifanye maamuzi ya haraka kuhusu marekebisho ya sheria hizo ili kuepusha kesi zaidi za kisheria.
Ligi Kuu ilikataa kutoa maoni zaidi lakini imesisitiza kuwa muhtasari wao ni sahihi na haukuwa na upotoshaji wowote.