Taa za vivuko (Traffic lights) hutumika sehemu za makutano ya barabara kwa ajili ya kuviongoza vyombo vya moto pamoja na watumiaji wengine wa barabara lakini kwa Mkoa wa Iringa bado taa hizo hazijawekwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na msongamano kama ilivyo kwa majiji kama Dar es salaam.
Kutokana na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Iringa ikiwa ni pamoja na Manispaa ya Iringa kuanza kuwa na msongamano, Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada amesema kuwa kwa kushirikiana na TANROADS wapo kwenye mchakato wa kufunga taa hizo za vivuko yaani traffic lights.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa, Mstahiki Meya amesema kuwa bado mchakato huo unaendelea kufanyika hivyo kila kitu kikikamilika taa hizo zitafungwa katika maeneo matatu ambayo yatateuliwa kufungwa.
Vile vile Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada amesema kuwa mpaka sasa jumla ya vikundi 90 vya wanawake katika Halmashauri yake tayari vimeomba mikopo ya asilimia 10 ambayo ilirejeshwa baada ya hapo awali kusimamishwa kwa sababu mbalimbali.
Sambamba na hayo, Meya amesema kuwa Serikali imetoa shilingi Milioni 917 za mikopo ya asilimia 10 na zinatarajiwa kupelekwa katika vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Hata hivyo, Meya Ngwada amewaagiza viongozi wa Kata zote za Manispaa ya Iringa kufuatilia na kusimamia fedha hizo za mkopo na kuhakikisha zinarudishwa kulingana na utaratibu uliowekwa