Kanisa Katoliki nchini Sudan Kusini linapanga kufanya maombi maalum Alhamisi kwa ajili ya kuwasili salama kwa Papa Francis ambaye anatarajiwa kuwasili nchini humo Ijumaa.
Papa Francis kwa sasa yuko katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambako aliongoza moja wapo ya ibada zenye idadi kubwa zaidi ya watu Jumatano, ambapo watu wapatao milioni walihudhiria katika mji mkuu, Kinshasa.
Maombi kwa ajili ya kuwasili kwa Papa nchini Sudan Kusini yatafanyika katika eneo la kaburi la rais wa zamani John Garang mjini Juba, amesema Askofu mkuuStephen Ameyu Martin.
“Ninataka kutoa tangazo hili kwa Wakristu wote, tuje sote hapa Alhamisi saa kumi na moja jioni (15:00 GMT) kuombea afya ya Babamtakatifu Papa Francis na kuwasili kwake salama katika nchi yetu Ijumaa,” Askofu Mkuu.
Balozi wa Vatican nchini Sudan Kusini, Askofu mkuu Hubertus van Megen, ataongoza ibada ya Misa.
Wakati huo huo, serikali inasema imewapeleka maafisa wa usalama 5000, wanajeshi na polisi kuimarisha hali ya usalama wakati wa ziara ya Papa.