Siku moja baada ya tukio la kitengo maalum cha jeshi la Guinea kutangaza kuupindua utawala wa Rais Alpha Conde na kumshikilia Rais huyo, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Marekani, Ufaransa na jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za magharibi mwa Afrika (ECOWAS) zimeshutumu vikali mapinduzi hayo na kutaka Rais Conde aachiliwe huru mara moja.
Taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi pamoja na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja huo Moussa Faki Mahamat, imelitaka Baraza la Usalama nchini Guinea kufanya kikao cha dharura ili kutathmini hali ilivyo na lichukue hatua muafaka.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia ameshutumu vikali hatua hiyo ya jeshi kuchukua madaraka kwa nguvu, kupitia ukurasa wa Twitter, Guterres ametaka Rais Conde kuachiliwa huru mara moja.
Vikosi maalum vya jeshi nchini humo vilidai kuupindua utawala wa Rais Alpha Conde ambaye ametawala Nchi hiyo kwa muda mrefu na kusema wanamshikilia Rais huyo.
Wakuu wa Mapinduzi hayo wametangaza marufuku ya Watu kutoka nje nchini kote hadi watakapotoa maelezo zaidi, pia wamesema nafasi za magavana sasa zimechukuliwa na wanajeshi na kusisitiza kuwa Conde yuko salama na hajajeruhiwa.
KAMANDA ALIEONGOZA MAPAMBANO YA KUMTOA RAIS CONDE AFUNGUKA “UFISADI ULIOKITHIRI USIMAMIZI MBAYA”