Baada ya Rwanda kutangaza mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg mnamo Septemba 27, Waziri wa Afya wa nchi hiyo amejaribu kuwahakikishia umma kuwa hali imedhibitiwa.
Katika kikao hicho na wanadiplomasia na wadau wa maendeleo, Waziri Nsanzimana alizungumzia mikakati ya chanjo inayowekwa ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Wiki iliyopita, Rwanda ilipokea dozi 700 za chanjo chini ya majaribio, ambayo imetolewa kwa wataalamu wa afya na wale ambao wameguswa na kesi zilizothibitishwa.
“Tulikuwa tumefahamishwa kuwa chanjo zinapatikana. Nadhani tulichukua kama fursa nzuri kuwa nazo na kuimarisha mfumo wetu wa kinga,” Augustin Sendegeya, Mganga Mkuu wa Hospitali ya King Faisal.
Ingawa chanjo hiyo bado iko chini ya majaribio, Sendegeya alisema anaamini kuwa ni salama na inaweza kuwa muhimu kwa wale ambao wako katika hatari ya kuambukizwa.
Madaktari wengine pia wamesisitiza kwamba hawajaona athari kubwa kutoka kwa chanjo hiyo. “Hata sitarajii mengi kwa sababu niliona watu waliochukua chanjo jana na hawakuwa na dalili nyingi,” alisema Blaise Dushimiyimana, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake katika Hospitali ya Kufundisha ya Chuo Kikuu cha Kigali.
Zaidi ya watu 200 nchini wamepokea chanjo hiyo kufikia sasa.
Ugonjwa wa virusi vya Marburg ni ugonjwa mbaya, ambao mara nyingi unaua, kwa wanadamu. Rwanda imeripoti kuwa watu 13 wamefariki kutokana na ugonjwa huo tangu kuzuka kwa ugonjwa huo.