Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema tangu Serikali ilipotangaza uwepo wa ugonjwa wa Marburg Mkoani Kagera March 21, 2023 hadi sasa, jumla ya Watu waliopata maambukizi ni tisa ambapo kati ya hao watatu wamepona akiwemo Daktari aliyewahudumia Wagonjwa wa mwanzo kabla ya kuthibitika huku Wagonjwa sita wakipoteza maisha akiwemo Mtumishi mmoja wa afya na Mtoto mmoja mwenye umri wa miezi 18.
Akitoa taarifa kuhusu mwenendo wa ugonjwa huo Nchini, Waziri Ummy amesema “March 21 2023 tulitoa taarifa ya uwepo wa Watu wenye Marburg, Kagera, nafurahi kuwajulisha kuwa kuanzia Aprl 21, 2023 hatuna Mgonjwa yeyote mwenye virusi vya ugonjwa huu Kagera, Wagoniwa wawili waliokuwa wamesalia katika vituo maalum vya matibabu waliruhusiwa kutoka tarehe 20 na tarehe 21 Aprili 2023 baada ya kuthibitika kuwa hawana tena Marburg”
“Aidha tokea April 4, 2023 nilipotoa taarifa yangu ya mwisho kwa umma kuhusu Mwenendo wa ugonjwa huu, tulipata ongezeko la mgonjwa mpya mmoja ambaye ni Mama wa Mtoto wa umri wa miezi 18 aliyekuwa ametengwa na baadaye kuthibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Marburg ,hii inaonesha kuwa hatua za haraka zilizochukuliwa na Serikali zilipelekea kuhakikisha ugoniwa huu hausambai nje ya Familia zilizoathirika na kwa watumishi wa afya”
“Vilevile, ninafurahi kuwajulisha kuwa Watu 211 kati ya Watu 212 waliokuwa wametangamana na wagoniwa na kuwekwa karantini wameruhusiwa baada va kumaliza siku 21 za ufuatiliaji bila kuonesha dalili za ugonjwa huu, hii ni ishara kuwa itihada za pamoja zilizofanyika katika kukabiliana na mlipuko huu zimeleta mafanikio makubwa”