Marekani ilitangaza Jumatatu kuwa itakataa kutoa viza kwa maafisa wa Uganda ambao wanatekeleza sheria tata ya kupinga ushoga iliyotungwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki mwezi Mei ambayo inajumuisha adhabu hadi ya kifo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema hatua hiyo itatumika kwa maafisa wa Uganda, wanaohudumu na wa zamani, na wanafamilia wao, ikiwa watapatikana kuwa na jukumu la “ukandamizaji wa watu waliotengwa au walio hatarini”.
“Makundi haya yanajumuisha, miongoni mwa mengine, watetezi wa mazingira, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari, watu wa LGBTQI+ na viongozi wa mashirika ya kiraia,” Blinken alisema katika taarifa.
“Kwa mara nyingine tena, ninahimiza sana serikali ya Uganda kufanya juhudi za kutetea demokrasia na kuheshimu na kulinda haki za binadamu, ili tuweze kudumisha ushirikiano wa miongo kadhaa kati ya nchi zetu mbili ambao umewanufaisha Wamarekani na Waganda pia,” aliongeza.
Mara tu sheria hiyo ilipopitishwa, Rais wa Marekani Joe Biden alitoa wito wa kufutwa mara moja na kutishia kupunguza misaada ya Marekani na uwekezaji nchini Uganda.
Sheria inatoa adhabu kali, hadi kifungo cha maisha au hata adhabu ya kifo, kwa watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja au “kukuza” ushoga.
Ingawa imejumuishwa katika sheria za Uganda, hukumu ya kifo haijatumika kwa miaka mingi.