Rais wa Marekani, Joe Biden ameishutumu sheria mpya ya Uganda ya kukabiliana na wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja akita yenye kutia aibu na ukiukwaji mbaya wa haki sawa za binadamu nchini Uganda.
Katika taarifa ya Jumatatu, rais Biden amesema sheria hiyo ndilo tukio la hivi karibuni katika hali inayotia mashaka ya ukiukwaji wa haki za binadamu na rushwa nchini Uganda.
Waziri wa mambo ya nje Antony Blinken anasema huenda Marekani ikafikiria kuwawekea vikwazo baadhi ya maafisa wa Uganda baada ya nchi hiyo kupitisha mojawapo ya sheria kali zaidi duniani dhidi ya LGBTQ.
Blinken alisema Marekani “imesikitishwa sana” na Sheria ya Uganda dhidi ya Ushoga, ambayo ilitiwa saini na Rais Yoweri Museveni kuwa sheria siku ya Jumatatu.
Wakati mahusiano ya watu wa jinsia moja yalikuwa haramu nchini Uganda, sheria mpya inatoa adhabu ya kifo kwa baadhi ya tabia ikiwa ni pamoja na “ushoga uliokithiri”, na miaka 20 jela kwa “kukuza” ushoga.
Hapo awali Museveni alikuwa amewataka wabunge kufuta kifungu cha “ushoga uliokithiri”.
Rais wa Marekani Joe Biden alilaani haraka sheria hiyo kama “ukiukaji mbaya wa haki za binadamu kwa wote” na kutishia kupunguza misaada na uwekezaji kwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Aliitaka Uganda kubatilisha hatua hiyo.
Katika taarifa yake baadaye Jumatatu, Blinken alisema Marekani “itazingatia kupeleka zana zilizopo za vizuizi vya viza dhidi ya maafisa wa Uganda na watu wengine binafsi kwa unyanyasaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki za binadamu za LGBTQI+
Mwongozo wa idara ya serikali kwa raia wa Marekani na wafanyabiashara wanaosafiri kwenda Uganda pia ulisasishwa, wakati Washington pia ingesaidia “kutayarisha mbinu za kuunga mkono haki za LGBTQI+ nchini Uganda na kukuza uwajibikaji kwa maafisa wa Uganda na watu wengine wanaohusika na, au kushiriki katika , kudhulumu haki zao za kibinadamu”, aliongeza.
Kundi la kutetea haki za binadamu lilitangaza baadaye Jumatatu kwamba liliwasilisha pingamizi la kisheria katika Mahakama Kuu ya Uganda, likisema kwamba sheria hiyo “ilikuwa kinyume cha katiba waziwazi”.
“Kwa kuharamisha kile tunachoita shughuli za kukubaliana za mapenzi ya jinsia moja miongoni mwa watu wazima, inakwenda kinyume na vifungu muhimu vya katiba ikiwa ni pamoja na haki za usawa na kutobaguliwa,” alisema Adrian Jjuuko, mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa la Uhamasishaji na Uendelezaji wa Haki za Binadamu.