Marekani imetoa onyo kali kwa serikali ya Iran kuhusiana na mipango yake ya kudhuru rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, na kusema kwamba shambulio lolote dhidi yake litaonekana kama kitendo cha vita.
Afisa mmoja wa Marekani, aliyenukuliwa kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema Jumatatu kwamba Rais Joe Biden amekuwa akifuatilia vitisho kutoka Iran kwa miaka mingi, na ameagiza timu yake kuchukua hatua za kukabiliana na mipango hiyo.
Afisa huyo alieleza kuwa maafisa wa ngazi za juu wa Marekani wamewasilisha ujumbe kwa serikali ya Iran, wakiwataka waache mara moja mipango yote ya shambulio dhidi ya Trump na maafisa wa zamani wa Marekani.
Kulingana na maelezo hayo, Marekani itachukulia jaribio lolote la kumdhuru Trump kama kitendo cha vita.
Iran imekanusha madai ya kuingilia masuala ya ndani ya Marekani, huku ikitaja matukio mbalimbali kama ushahidi wa kuingiliwa kwake na Marekani, yakiwemo mapinduzi ya 1953 na mauaji ya kamanda wake mkuu, Qassem Soleimani, mwaka 2020.
Trump aliamuru shambulio la anga lililomuua Soleimani baada ya kupata taarifa za kijasusi kwamba alikuwa anapanga mashambulizi dhidi ya wanadiplomasia na vikosi vya Marekani Mashariki ya Kati.
Katika kampeni yake ya kurudi Ikulu, Trump amekuwa akipokea taarifa za vitisho kutoka Iran, huku White House ikisisitiza kuwa Marekani itaichukulia hatua kali Iran iwapo shambulio lolote litafanyika dhidi ya raia wake.