Watoto ni miongoni mwa waliofariki baada ya shambulizi la anga la Israel kwenye jengo moja katika kambi ya wakimbizi ya Gaza kuwaua takriban watu 33, kulingana na mamlaka ya afya inayoendeshwa na Hamas.
Shambulio hilo – ambalo Israel ilisema lililenga “gaidi mkubwa” lakini huenda lilisababisha mlipuko wa pili – lilikuja saa chache baada ya mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani kuibua matumaini ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Zaidi ya watu 80 wanasemekana kupotea baada ya shambulizi katika kambi ya Nuseirat usiku wa Alhamisi.
Madaktari wa Kipalestina pia waliripoti zaidi ya watu 40, wengi wao wakiwa watoto, walikuwa wakipokea matibabu katika hospitali mbili, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha jengo lililoporomoka, ambalo Reuters inaripoti kuwa lilikuwa ni ofisi ya posta iliyotumika kama makazi.
Hospitali ya al Aqsa imesema shambulio hilo pia liliharibu nyumba kadhaa za jirani.
Nuseirat ni moja ya kambi nane za kihistoria huko Gaza, ambazo asili yake zilikuwa za wakimbizi wa Kipalestina kutoka vita vya 1948 vilivyopelekea kuanzishwa kwa Israeli.
Sasa ni sehemu ya eneo la mijini lenye watu wengi waliofurushwa kutoka Gaza.