Halmashauri ya Mji wa Geita imeendelea kupata Mafanikio Makubwa kupitia Michezo mbalimbali ya Mpira wa Miguu ambayo imekuwa ikiendeshwa na Mradi wa Kuwezesha Mabinti Balehe kuendelea na Masomo licha ya kuwepo kwa sababu mbalimbali ambazo zimekuwa zikitajwa na waratibu wa Mashindano hayo.
Hayo yamesemwa na Afisa Maendeleo kata ya Kalangalala Costantine Lucas Baada ya kukamilika kwa Mashindano ya Mpira wa Miguu uliofanyika na kuchezwa katika uwanja wa Kata ya Ihanamilo Halmashauri ya Mji wa Geita ambapo amesema Mashindano haya yaliyoandaliwa na KAGS yamesaidia kuwafikia walengwa kwa uharaka zaidi na kutatua changamoto zao.
Lucas amesema imekuwa ni rahisi kupata taarifa za matukio ya ukatili tofauti na zamani ukilinganisha na hapo awali huku akiwataka wazazi pamoja na walezi kuacha tabia ya na kuwatukana na kuwaita Majina ya wanyama huku akisema matukio ya ukatili yamekuwa yakikithiri hasa maeneo ya vijijini.
“Changamoto kubwa ni hiyo ambayo ukatili wa kimwili nafikiri unafanyika changamoto kwao lakini pia wakati mwingine kwenye Familia zetu tunaona ukatili wa kihisia au kisaikolojia pale ambapo Baba na Mama anatumia zile lugha za Matusi na Vitisho unakuta inaathiri watu lakini kwasababu kupitia elimu hii najua haya matukio yataendelea kupungua zaidi, ” Afisa Maendeleo Lucas.
Kwa upande wake Mratibu wa Msaidizi wa Mashindano Azori Balosha amesema lengo la mashindano hayo ni kutoa ujumbe na elimu kwa mtoto wa kike katika kumsaidia mtoto wa kike kuondokana na changamoto za ukatili katika Jamii inayowazunguka huku akisema Michezo hiyo imesaidia sana kupinga vitendo vya kikatili kwenye Jamii.
Amesema KAGS wamekuwa wakiendelea kushirikiana na Serikali katika kuona mtoto wa kike anarudishwa shuleni pamoja na kupinga vitendo vya kikatili ambavyo vimekuwa vikifanywa na Jamii huku michezo pamoja na majukwaa ikiwa ni sehemu ya Jamii kujifunza.
Stelius Abas ni Kaimu Afisa Mtendaji kata ya Ihanamilo amesema kabla ya Mashindano hayo elimu ya ukatili ilikuwa haiifikii Jamii kwani Njia ambazo zilikuwa zinatumika zilikuwa hazimfikii mwananchi moja kwa moja huku akisema uwepo wa mashindano ya Mpira wa Miguu yamesaidia kwa asilimia 90 kukomesha vitendo vya ukatili kwa mtoto wa kike.