Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, alikutana na viongozi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Alhamisi ili kujadili mlipuko wa ugonjwa wa mpox unaoendelea kuathiri taifa hilo.
Mkutano huo ulilenga kusisitiza mwitikio wa pamoja katika kukabiliana na mlipuko huo, hasa katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ambako kuna migogoro.
Dk. Tedros alieleza kupitia Mtandao wa X kwamba mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha juhudi zinazoongozwa na serikali, ikiwemo kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa, kuongeza uelewa kwa jamii, na kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa wagonjwa muhimu na wale waliokaribiana nao.
“Tulikubaliana kwamba kwa kuchukua hatua kwa pamoja na kuratibu vizuri, tunaweza kudhibiti mlipuko wa mpox,” alisema Dk. Tedros.
WHO imeutaja ugonjwa wa mpox kama dharura ya afya ya umma inayohitaji uangalizi wa kimataifa, huku zaidi ya visa 15,000 vikishukiwa katika nchi 12 za Afrika.
DRC, ikiwa kitovu cha mlipuko, pamoja na Burundi na mataifa mengine ya Afrika Mashariki, yanatarajiwa kupokea chanjo hivi karibuni, kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC).
SOURCE