Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya leo Juni 1.2022 amefikishwa katika Mahakama ya hakimu Mkazi Moshi Mkoani Kilimanjaro akiwa na wenzake watano kwa makosa saba ya uhujumu uchumi.
Akisoma mashtaka hayo yanayomkabili Sabaya na wenzake, Mwendesha mashataka wa Serikali Tumaini Kweka amesema kuwa Sabaya na wenzake wanne Sylvester Nyegu, John Odemba Aweyo,Nathan Msuya na Antheo Boniface Assey wanashtakiwa na makosa saba ya uhujumu uchumi ikiwemo kuongoza genge la uhalifu, kutenda kinyume na mamlaka yake, kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na utakatishaji wa fedha haramu.
Hata hivyo Wakili upande wa utetezi Hellen Mahuna ameiomba Mahakama hiyo kufuata sheria ili kutenda haki akidai kuwa wateja wake na Mahakama ya Arusha haikupata kibali halali cha kuwatoa washtakiwa gereza la Kisongo Arusha na kuwapeleka gereza la Karanga Moshi.
Kwa upande wake Sabaya aliyeomba kuongea licha ya Hakimu kueleza kuwa maombi yake hayatazingatiwa kwa sasa alieleza mahakamani hapo kuwa hana imani na Mwendesha mashtaka wa serikali Tumaini Kweka.
Sabaya akiwa anatokwa na machozi mahakamani amesem hana imani na Mwendesha mashtaka wa serikali Tumaini Kweka kwa kuwa anatokea Wilaya ya Hai Kijiji cha Makoa nilipo kuwa nafanyia kazi, anatumikaa kisiasa na anachuki, nakuomba Rais Samia alione hili linalofanyika Kilimanjaro katika kesi hiyo na kwamba hao anaoshtakiwa nao wanateseka bure pamoja na yeye ikiwa Kweka ataendelea na kesi hiyo
Kufuatia mabishano hayo Hakimu Mkazi Mfawidhi aliyekuwa anasikiliza shauri hilo Salome Mshasha aliahirisha usikilizaji wake kwa muda wa dakika kumi (10) ili apate kupitia sheria juu ya yaliyotajwa huku akidai kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayo mkabili Sabaya na wenzake.
Kesi ya hiyo ya uhujumu uchumi namba 2 ya mwaka 2022 imeahirishwa hadi Juni 7,Mwaka huu na Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi Moshi,Salome Mshasha.