Wabunge wameitaka serikali kulipa fidia kwa wafanyabiashara waliopoteza mali zao kutokana na ajali za moto ambazo siku za hivi karibuni zimezuka katika masoko mbali mbali nchini.
Pia wameitaka serikali kuongeza magari ya zima moto ili kuwa na vifaa vya kutosha vitakavyowawezesha kukabiliana na matukio hayo.
Mbunge wa viti maalum, Cecili Paresso akizungumza bungeni leo Mei 10, 2022 alihoji nini kauli ya Serikali juu ya matukio ya moto katika masoko nchini.
Aidha, katika swali la nyongeza amehoji kwanini Serikali isiwalipe fidia wananchi walioharibiwa bidhaa zao kutokana na ajali hizo hasa ikizingatiwa Serikali inakusanya kodi na tozo mbalimbali kwao.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amesema kuhusu suala la fidia ni suala la kisheria na hadi sasa hamna sheria inayoilazimu serikali kulipa fidia kwenye matukio ya ajali za moto.
Akizungumzia matukio hayo ya moto, Sagini amesema uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine umebaini sababu mbalimbali za matukio hayo.
Ametaja sababu hizo ni pamoja na uunganishwaji holela wa mifumo ya umeme, kutokuzingatia tahadhari za moto kwa mama lishe na baba lishe na shughuli za uchomeleaji holela wa vyuma katika masoko.
“Katika kukabiliana na vyanzo vya matukio hayo umefanyika ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto sambamba na utoaji wa elimu na mafunzo ya matumizi ya vifaa vya awali vya kuzima moto katika masoko nchini,” amesema.