Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la kimataifa la hisani la Oxfam imesema ukwasi wa watu 10 walio matajiri zaidi duniani umeongezeka marudufu katika muda wa miaka miwili ya mwanzo ya janga la virusi vya corona wakati hali ya umasikini na ukosefu wa usawa ikizidi makali kote duniani.
Katika ripoti hiyo Oxfam imesema utajiri wa watu hao 10 umefikia dola za kimarekani trilioni 1.5 kutoka dola bilioni 700 miaka miwili iliyopita.
Oxfam imeutaja ukosefu huo wa usawa kuwa “uhalifu wa kiuchumi” na kwamba unachangia vifo vya watu 21,000 kila siku kutokana na ukosefu wa huduma za afya, unyanyasaji wa kijinsia, njaa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Shirika hilo limezitaka serikali duniani kuchukua hatua nzito kukabiliana na ukosefu mkubwa wa usawa ikiwa ni pamoja na kuwatoza zaidi matajiri na kuyadhibiti makumpuni makubwa.