Jeshi la Polisi nchini kupitia kamisheni ya polisi jamii, limekuja na mbinu ya kuzuia matukio ya uhalifu hususani ya mauaji pamoja na ukatili kabla hayajatokea kwa kuwatumia wakaguzi wa polisi ambao wamepangwa katika Kata zote nchini.
CP Shilogile amebainisha kuwa hivi karibuni kumeibuka matukio ya mauaji na ya ukatili wa kijinsia ambapo amesema sababu zikiwa ni pamoja na imani za kishirikina, migogoro ya ardhi pamoja na wivu wa mapenzi.
Kamishna Shilogile aliendelea kufafanua kuwa wakaguzi hao kupitia mafunzo mbalimbali waliyopewa wataenda kubaini viashiria vya uhalifu, kushauri na wakati mwingine kutoa taarifa mapema ili hatua za haraka zichukuliwe kabla ya uhalifu kutokea.
Aidha amewataka Askari wote nchini kwenda kushirikiana na viongozi wa serikali, wazee wa mila pamoja na viongozi wa dini ili wote kwa pamoja wakemee vitendo hivyo pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili kukomesha matukio hayo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo, pamoja na kushukuru maelekezo na elimu waliyoipata kupitia kikao hicho amesema jeshi hilo mkoani humo litakwenda kuboresha utendaji wake wa kazi hali ambayo itapelekea kuwa na matokeo mazuri ndani ya taasisi na jamii yote kwa ujumla.