Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wanatarajiwa kukutana hivi karibuni kwa ajili ya kujadili virusi vya homa ya MPOX ambavyo vinaenea kwa kasi sasa katika maeneo tofauti ya dunia.
Katibu Mtendaji wa SADC Elias Magosi amesema kuwa, mkutano wa mawaziri wa afya utaitishwa ili “kuwezesha utaratibu wa kukabiliana na ugonjwa huo, ambao umeenea katika zaidi ya nchi kumi za Afrika.
Wiki iliyopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliitangaza Mpox kuwa “dharura ya afya ya umma” kwa mara ya pili sasa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Kabla ya hapo pia, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika CDC kilitangaza “dharura ya afya ya umma”, kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari, juu ya mripuko wa Mpox unaoenea kwa kasi katika bara hilo, na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kukomesha kusambaa kwake.