Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Makame Mbarawa ameisifu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) kwa utekelezaji wa ujenzi wa bandari mpya na ya kisasa ya Mbamba Bay inayojengwa pembezoni mwa Ziwa Nyasa katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma; akisema kuwa ujenzi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha bandari mbalimbali hapa nchini.
Akizungumza baada ya kutembeleo eneo la mradi huo wenye thamani ya bilioni 75.8 wilayani humo hapo jana, Waziri Mbarawa amesema ujenzi wa bandari hiyo utasaidia usafirishaji wa haraka wa mizigo, zikiwemo bidhaa za viwandani, mazao ya kilimo na uvuvi mizigo kwenda nchi jirani za Msumbiji, Malawi, na Zambia zikitokea bandari ya Mtwara kupitia Ziwa Nyasa.
“Naipongeza sana TPA kwa ujenzi wa bandari hii ya aina yake kujengwa katika ukanda huu wa Ziwa Nyasa,”
“Ujenzi huu, mbali na kutoa ajira, pia utakuza uchumi wa nchi yetu na nchi za jirani zinazotumia bandari hii kusafirisha mizigo yao,” amesema Waziri Mbarawa.
Amesema dhamira ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kujenga miundombinu ya kisasa katika bandari zote hapa nchini, ili kukuza uchumi na kutoa ajira kwa Watanzania.
Hivyo, ameitaka TPA kusimamia vizuri ujenzi wa bandari hiyo kwa kushirikiana na Mshauri na Mkandarasi wa mradi ili umalizike katika muda uliopangwa na kuanza kutoa huduma.
Akizungumza wakati wa kutoa maelezo ya mradi huo kwa Waziri, Mkurugenzi Msaidizi wa TPA Juma Kijavara amesema kuwa ujenzi wa bandari hiyo mpya ya kisasa utahusisha pamoja na mambo mengine,ujenzi wa gati mbili zenye urefu wa mita 103 zenye uwezo wa kuhudumia meli mbili kubwa, tofauti na uwezo wa bandari ya sasa ambayo inahudumia zaidi boti ndogo za kubeba mizigo na abiria.
Pia ujenzi wa bandari mpya utahusisha pia ujenzi wa maghala, nyumba za watumishi, jengo la utawala, jengo la abiria, karakana, mnara wa tanki la maji na jengo la huduma za afya.
Pia kutakuwa na ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 105 na upana wa mita 15 kwa ajili ya magari ya kubebea mizigo na eneo la kuhifadhia makontena 3,000 ya mizigo.
Ujenzi pia utahusisha barabara za ndani na nje ya bandari kwa ajili ya magari kuingia na kutoka bandarini hapo.
Awali, Mhandisi wa mradi huo kutoka TPA John Paul amesema kuwa mpaka sasa hatua ya utekelezaji wa mradi huu imefika asilima 6, ambapo kazi zilizofanyika na ambazo zinaendelea ni pamoja na Usanifu wa Kihandisi, maandalizi ya eneo la ujenzi, ujenzi wa majengo ya ofisi za Mkandarasi na Mhandisi Mshauri, pamoja na kuleta vifaa na mitambo itakayotumika wakati wa ujenzi.
Pia amemfahamisha Waziri Mbarawa kuwa mpaka sasa, TPA imeshamlipa mkandarasi mjenzi malipo ya awali (Advance Payment) kiasi cha shilingi 3,261,529,017.63 sawa na asilimia 5 na kumlipa Mhandisi Mshauri kiasi cha shilingi 448,192,240.70 kama malipo ya awali ambayo ni sawa na asilimia 10.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPA , ukilinganisha na miaka ya nyuma, ujenzi wa bandari mpya utaongeza ufanisi, ikiwemo idadi ya shehena za mizigo na abiria wanaotumia Ziwa Nyasa.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita (yaani mwaka 2021/22, 2022/23 na 2023/24), utendaji kazi wa bandari za Ziwa Nyasa kwa ujumla umekuwa ukiongezeka ambapo kwa mwaka 2021/22, idadi ya mizigo ilikuwa tani 5,410 na idadi ya abiria ilikuwa watu 2,437.
Pia kwa mwaka 2022/23, idadi ya mizigo ilikuwa tani 11,351.40 na abiria walikuwa 70,172 na mwaka 2023/24 mizigo ilikuwa tani 2,619.56 na abiria walikuwa watu 15,194.
Hivyo, katika kipindi cha miaka mitatu , jumla ya mizigo yote iliyosafirishwa katika bandari hizo za Ziwa Nyasa ni tani 19,380.96 na abiria ni 87,803, huku tathmini ikionyesha kuwa shehena kubwa ilitoka bandari ya Mbamba Bay ukilinganisha na bandari ya Kiwira pamoja na nyingine za ukanda huu.
Kwa mujibu wa TPA, miongoni mwa faida za ujenzi wa bandari mpya ni pamoja na ajira kwa vijana wanaozunguka mradi, fursa za biashara ikiwemo huduma ya chakula kwa mkandarasi na wafanyakazi, kukuza biashara na uchumi kikakanda na kimataifa kwa kuiunganisha Tanzania na nchi jirani, kuhamasisha uwekezaji, hususan katika sekta ya viwanda na biashara.
Ujenzi wa bandari hiyo mpya unasimamiwa na Mkandarasi Xiamen Ongoing Construction Group Limited na mshauri (Consultant) Anova Consult na unatarajiwa kukamilika Januari 26, 2026.