MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile amesema juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kilimo zinaonyesha utayari wake kuiletea maendeleo sekta hiyo.
Ditopile ameyasema hayo leo Agosti 18, 2023 katika mkutano mkuu wa wadau wa korosho ambapo ametaja moja ya maeneo ambayo Rais Samia ameweka nguvu ni kuongeza Bajeti ya kilimo kila mwaka.
“Imekuwa hadithi, umekuwa wimbo tunaouimba hata huko bungeni kwamba uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu ni kilimo, asilimia kubwa ya Watanzania wamejiajiri katika kilimo, lakini imeendelea kuwa hadithi na maneno.
“Lakini mwanamama huyu shupavu anayeamini katika kilimo tangu ameingia madarakani kule bungeni tunaletewa bajeti kubwa na sisi tunaipitisha kwa kauli moja, hongera sana mheshimiwa Rais,” amesema.
Ditopile aliwaeleza Wadau hao wa Kilimo kuwa wabunge hususan wanaotoka katika Mikoa inayolima korosho wataendelea kusimama imara kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuimarika na kumletea tija kubwa zaidi mkulima na wote wanaounda mnyororo wa kilimo.
“Nataka niwatoe hofu na kuwapa imani wadau wote wa kilimo nyie mnakutana mara moja kwenye mkutano huu, lakini sisi wadau wenzenu wa kilimo tunalala na kuamka na wizara ya kilimo kwa niaba yenu…watieni moyo wabunge wote wakiongozwa na wabunge wanaotoka mikoa inayolima korosho na sisi kama kamati inayohusika na maendeleo ya kilimo tutayachukua yanayojadiliwa hapa na kwenda kuyafanyia kazi,” amesema.