Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni leo amewasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2023/2024 ambapo moja ya mambo aliyoyasema kwenye hotuba yake ni kupungua kwa matukio 448 ya ajali za barabarani nchini.
Masauni amesema “Hali ya usalama barabarani imeendelea kuimarika kutokana na Polisi
kuendelea kusimamia Sheria za Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Wadau ambapo katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023 matukio ya ajali 1,283 yaliyotolewa taarifa ikilinganishwa na matukio 1,731 yaliyotolewa taarifa katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22 ikiwa ni kupungua kwa matukio 448 sawa na 25.9%”
“Kupungua kwa matukio ya ajali kunatokana na kuimarisha usimamizi wa sheria, kufanyika kwa operesheni maalum, doria na misako Nchi nzima, aidha elimu ya usalama barabarani imeendelea kutolewa kwa makundi yanayotumia barabara, matukio ya ajali yalisababisha Watu 1,893 kujeruhiwa katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023 ikilinganishwa na Watu 2,323 waliojeruhiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22, idadi ya majeruhi imepungua kwa Watu 430, sawa na
18.5%”
“Aidha, matukio hayo yalisababisha vifo 842 katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023 ikilinganishwa na vifo 946 katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22, idadi ya vifo imepungua kwa watu 104, sawa na 11%”