Mbunge wa Jimbo la Kijini, Yahya Khamis Ali (Mambalesi) amekabidhi msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na Taasisi ya Human bridge ya nchini Sweden.
Vifaa hivyo, vyenye thamani ya shilingi milioni 600 za Kitanzania, vinajumuisha vitanda na magodoro ya kulalia wagonjwa, baskeli za watu wenye ulemavu, mashuka, nguo, na vifaa vingine vya hospitali.
Baada ya kukabidhi vifaa hivyo hafla iliofanyika uwanja wa mpira Good hope Kivunge Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Mambalesi alisema msaada huo ni matokeo ya maombi yake kwa balozi wa Sweden na umeletwa kama hatua ya kusaidia kutatua changamoto za afya na kuwa vitasambazwa katika hospitali zote za jimbo lake ili kuboresha huduma na kupunguza uhaba wa vifaa katika maeneo hayo.
Aidha, alisisitiza kuwa atashirikiana na viongozi wengine wa jimbo hilo ili kuendelea kutafuta wadau na wafadhili watakaosaidia kuleta maendeleo zaidi kwa wananchi, huku akiwapongeza Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Husein Ali Mwinyi kwa juhudi zao katika kuboresha maisha ya Watanzania.
Mbali na Hayo alitangaza kuwa sasa ameteuliwa kuwa balozi wa Taasisi ya Human Bridge nchini Tanzania na atahakikisha vifaa vyote vya hospitali vitakavyotolewa vitafika kwa wakati na kutowa kipaumbele kwa wananchi wa jimbo lake.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A, Machano Fadhil Machano (babla), alipongeza juhudi za mbunge huyo na kumshauri kuendelea kutafuta maendeleo katika sekta nyingine kama elimu na michezo.
Babla alieleza kuwa kwa kiasi kikubwa msaada huo utaleta mabadiliko chanya katika upatikanaji wa huduma za afya ndani ya jimbo la kijini na mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ujumla na kuwaasa madaktari dhamana kusimamia matumizi sahihi ya vifaa hivyo na kuvitunza ili vitumike kwa muda mrefu kwa maslahi ya taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Human Bridge Sweden, Bahat Kitoh, alimpongeza Mambalesi kwa juhudi zake na kusema kuwa hatua alizochukua zinapaswa kuigwa na viongozi wengine.
Aliongeza kuwa Taasisi hiyo itaendelea kutoa msaada wa vifaa tiba kwa Tanzania, ambapo hadi sasa kontena 40 za vifaa hivyo zimeshafika katika maeneo ya Tanzania Bara, ikiwa ni sehemu ya msaada wa Taasisi kwa serikali ya Tanzania