Mchezaji mpira wa Israel ambaye alionyesha ujumbe unaorejelea vita vya Israel na Hamas wakati wa mechi ya ligi ya daraja la kwanza nchini Uturuki amekamatwa, vyombo kadhaa vya habari vya Uturuki viliripoti Jumapili jioni.
Hapo awali, waziri wa sheria wa nchi hiyo alisema inamchunguza mchezaji wa Israel Sagiv Jehezkel kwa tuhuma za “uchochezi wa chuki”. Klabu yake ya Antalyaspor, tayari imemfuta kazi kutokana na tukio hilo.
Jehezkel, 28, na kufungwa mara nane na timu ya taifa ya Israel, alisherehekea kufunga bao dhidi ya Trabsonspor kwa ishara ya ujumbe ulioandikwa kwenye bendeji kwenye mkono wake wa kushoto, uliosomeka “siku 100. 07/10”.
Ujumbe huo ulionekana kuwa unarejelea siku 100 za vita vya Israel na Hamas, vilivyochochewa na shambulio la Oktoba 7 la Hamas kusini mwa Israel ambapo takriban watu 1,140 waliuawa na wengine karibu 250 walitekwa nyara.