Waendesha mashtaka wa Kenya wanasema kuwa Paul Mackenzie na wengine 94 watashtakiwa katika mahakama ya Malindi siku ya Jumatano.
Mtu huyo aliyejitangaza kuwa mchungaji amekana kuhusika na vifo hivyo.
Miili ya watu 429, wakiwemo watoto, imefukuliwa kutoka maeneo ya makaburi huko Shakahola, msitu ulio mbali ya takriban saa mbili kwa usafiri wa kutumia gari eneo la magharibi mwa mji huo.
Bw Mackenzie anadaiwa kuwahimiza waumini wa Kanisa lake la Good News International kuhamia huko na kujitayarisha kwa mwisho wa dunia.
Shahidi mmoja aliambia BBC kwamba watu walipewa maagizo Januari mwaka jana waanze kufunga ili “wafike mbinguni”.
Lakini Bw Mackenzie amesema hahusiki na vifo hivyo kwani alifunga kanisa lake mwaka wa 2019.
Wapelelezi walikuwa wameomba muda wake rumande uongezwe mara kadhaa huku wakiendelea na uchunguzi wao.
Walisema uchunguzi wao kwa sasa umekusanya ushahidi wa kutosha kumshtaki yeye na wengine kwa makosa ya mauaji, shambulio na “kuwezesha kutendeka kwa kitendo cha ugaidi”.
Kati ya washukiwa hao 95, 64 walipatikana Shakahola na awali walitibiwa kama waathiriwa na kuhamishiwa hadi katika kituo cha uokoaji.
Hata hivyo, wachunguzi baadaye waligundua kwamba wengi wao walikuwa na watoto waliokufa msituni na baadhi yao walikuwa wametoa majina na utambulisho wa uwongo na hawakuwajibikia watoto wao.