Mkuu wa wilaya Uvinza Dinnah Mathaman amesema kuwa mdau yeyote wa elimu anayetaka kumchukua mtoto Shauri John aliyetrend kwenye mitandao ya kijamii ambaye anataka kumchukua mtoto huyo kutoka kwa wazazi wake ili amsomeshe anapaswa kufuata taratibu za kisheria za kumkuchukua mtoto huyo ikiwemo kupata ridhaa ya wazazi na kibali cha serikali wilayani humo.
Mathamani alisema hayo akitoa maelekezo ya serikali kufuata wadau Zaidi ya 200 waliojitokeza kutaka kumchukua mtoto huyo akiwemo Mkuu wa wilaya Kisarawe mkoani Pwani, Petro Magoti baada ya kumuona mtoto huyo akizungumza @ayotv_ akieleza kiu yake ya kutaka kusoma badala ya kuchunga mifugo ya wazazi wake kama anavyofanya sasa hivi.
Akizungumza katika shule ya Msingi Kahwibili iliyopo kijiji cha Kahwibili kata ya Rukoma wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma Mkuu huyo wa wilaya Uvinza alisema kuwa serikali haimzuii mdau yeyote kumchukua mtoto huyo lakini amesisitiza kuwa lazima ridhaa wazazi na kibali cha serikali vifuatwe ili kuzingatia usalama wa mtoto huyo mahali atakapokuwa.
Katika hatua nyingine Mathamani amemuelekeza Afisa Elimu wa Wilaya hiyo kuboresha Ikama ya walimu katika Shule ya Msingi Kawibili yenye jumla ya walimu watatu jambo ambalo Afisa Elimu huyo ameahidi kulitekeleza kwa kuongeza walimu watatu ndani ya Siku 14 kuanzia Februari 19,2025.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewashukuru wote waliofanikisha kuibuliwa kwa taarifa za mtoto huyo sambamba wale wote wenye dhamira ya kumsaidia, huku akisisitiza zoezi ka upokeaji wa michango kwa sasa linaratibiwa na ofisi yake likisimamiwa na Mkurugenzi mtendaji wa Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Katibu Tawala Wilaya.