Magazeti

Waziri atoa saa 48 kwa RC Mwanza, Jk na Samatta, Serikali yafuta umiliki wa mashamba..#MAGAZETINI

on

MWANANCHI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete amempongeza mwanasoka bora wa Afrika, Mbwana Samatta kwa mafanikio aliyopata na sasa amemtaka alenge kucheza ligi kubwa za Ulaya ili Watanzania waweze kumuona kila Jumamosi kupitia kwenye luninga.

Kikwete ambaye ni Rais mstaafu amesema tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika aliyoipata itasaidia kutangaza soka ya Tanzania, kuwapa ari wachezaji wengine na kuwapa furaha Watanzania ambao wamekuwa na kiu ya kuona nchi inafanya vizuri zaidi.

“Angalau Mbwana ametuinua kwenye soka. Ametupa ari mpya. Ametupa furaha,Binafsi nampongeza kwa mafanikio,” alisema Kikwete alipotembelewa na mwanasoka huyo jana kwenye ofisi za CCM, Lumumba, Dar es Salaam.

“Narudia maneno niliyomuambia tulipokutana pale Kinshasa (DRC); alenge juu zaidi, shabaha iwe kucheza Ligi Kuu za Ulaya.

Tunapenda kila Jumamosi tukiangalia kwenye luninga tumuone Mbwana anatikisa nyavu, ni jambo la fahari, namtakia kila la kheri,” alisema Kikwete.

Kikwete hakusita kuonyesha furaha yake juu ya mafanikio hayo ya Mbwana na kusema Tanzania kwa muda mrefu imekosa furaha na imejawa na ukame wa makombe. “Baba yake alikuwa mwanamichezo, mshale umerudi kule kule,” alisema na kuongeza: “Waziri wa Michezo (alimgeukia Nape Nauye) naomba muangalie namna ya kumsaidia kijana huyu afike mbali zaidi.” Mbwana ambaye ni mchezaji wa klabu ya TP Mazembe ya DRC Alhamisi iliyopita alitwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa Wachezaji wa Barani Afrika katika hafla iliyoandaliwa Lagos, Nigeria.

Aidha, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa Mtanzania wa kwanza na mchezaji wa kwanza kutoka nchi za Afrika Mashariki kunyakua tuzo hiyo baada ya kuiongoza TP Mazembe kutwaa ubingwa wa Afrika yeye akipachika nyavuni mabao sita. Klabu kadhaa maarufu za nchi za Ulaya zinataka kumsajili, lakini tayari FC Genk ya Ubelgiji imekwishanasa saini yake.

Akizungumza katika ziara hiyo Mbwana alisema: “Siri kubwa ya ushindi ni nidhamu na kujituma. Lakini kubwa zaidi lililonipa changamoto ya kuhakikisha ninaongeza bidii zaidi kwenye kazi yangu ni pale nilipokutana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete pale Kinshasa.

Tulizungumza mambo mengi nikiwa na mwenzangu Thomas Ulimwengu, lakini kubwa alituasa tusikubali kubaki Afrika tujitahidi kwenda kucheza Ulaya.” “Nakumbuka Rais Kikwete alituambia maneno haya, tumeonyesha njia tusikubali kubakia Afrika tujitahidi kwenda kucheza Ulaya ili kuonyesha njia kwa vipaji vingine ambavyo viko nyumbani.

Alisema ninyi ndiyo alama ya mfano, Watanzania karibu wote tunawategemea kwenye medani ya soka. Mjitahidi msituangushe,” alisema.“Maneno haya kwa kiasi kikubwa yalinisukuma kuona ikiwa Rais anasema hivi, je familia yangu au watu wa karibu na sehemu niliyotokea wanachukuliaje hili suala, ilinipa ari na inabidi nifanye vizuri. Nashukuru Mungu amenisaidia,” aliongeza.

Alisema anaiweka tuzo hiyo kwa heshima ya Kikwete na kumuahidi kufika mbali zaidi. “Naomba baraka zake. Naomba Watanzania wazidi kuniombea,” alisema na kumkabidhi Kikwete jezi namba tisa yenye jina lake ‘Mbwana Samatta.

MWANANCHI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema Serikali imefuta umiliki wa mashamba 17 ambayo hayajaendelezwa katika Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na viongozi wa mkoa huo, Lukuvi alisema Serikali imefuta mashamba hayo baada ya mkoa kutoa mapendekezo ya kutaka yafutwe kwa sababu hayajaendelezwa. “Baada ya kupata mapendekezo ya mkoa tumefuta miliki ya mashamba lakini wamiliki ni wananchi wa kawaida, mbona vigogo wenye mashamba yasiyoendelezwa hamjawagusa, mnawaogopa? ” aliwahoji viongozi hao.

Lukuvi aliagiza ukaguzi ufanyike kwenye mashamba yote mkoani na kutoa mapendekezo kwa wizara ili yafutwe bila kuangalia cheo wala rangi ya mtu.

Alisema migogoro ya ardhi haiwezi kumalizika kama viongozi watakuwa wanafanya kazi kwa kuangalia vyeo vya watu. “Msimuogope mtu hata kama ni kigogo lakini msimuonee mtu, tendeni haki,” alisema.

Lukuvi alisema kuna wamiliki 35 wa mashamba mkoani humo ambao wametumia hati za mashamba hayo kukopa mamilioni ya fedha benki, lakini fedha hizo wamezitumia kwenye miradi mingine isiyo na uhusiano wa mashamba hayo.

Alisema pamoja na kukopa fedha hizo, lakini mashamba waliyotumia kupata mikopo wameyatelekeza bila kuyaendeleza. “Wako watu wamekopa kwa kutumia mashamba ya Mkoa wa Pwani lakini fedha walizopata wamekwenda kujenga nyumba za kupangisha Kigamboni (Dar es Salaam) na mashamba hawayaendelezi tutawanyang’anya,” alisema.

Lukuvi alisema atatoa orodha ya watu hao kwa uongozi wa mkoa ili uweze kuyakagua na kutoa taarifa kwa wizara. “Hatuwezi kuwatajirisha watu wa Dar es Salaam kwa kutumia mashamba ya Mkoa wa Pwani,” alisema.

Lukuvi alitoa orodha ya mashamba 50 ambayo yamenunuliwa kwenye vijiji vya mkoa huo, lakini hayajaendelezwa na kusababisha migogoro ya ardhi.

“Kutoendeleza mashamba kunasababisha migogoro ya ardhi kwani hivi sasa kuna watu wanayavamia,” alisema. Bei elekezi ya viwanja Waziri alisema wizara itatoa bei elekezi katika uuzaji wa viwanja kwa lengo la kupunguza bei. Alisema hivi sasa halmashauri zimekuwa zikichukua mashamba na kupima viwanja na kuviuza kwa mamilioni ya fedha ambayo si rahisi kwa mwananchi wa kawaida kumudu.

Alisema matokeo yake, viwanja hivyo vimekuwa vikinunuliwa na matajiri kwa malengo ya kuviuza kwa bei kubwa huku watu wa kawaida wakiendelea kujenga kwenye maeneo yasiyopimwa. “Halmashauri msifanye biashara katika viwanja, hii ni huduma sasa tunaweka bei elekezi ili kila mwananchi aweze kununua,” alisema.

Alizitaka halmashauri zilizochukua mashamba ya watu na kuyapima viwanja kuwalipa fidia kabla ya Juni. Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mgeni Baruani alimueleza waziri kwamba mkoa huo una migogoro ya ardhi hasa zile zinazopakana na Mkoa wa Dar es Salaam.

MWANANCHI

Kuna kila dalili kwamba mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar yamevurugika baada ya wahusika wakuu wa pande mbili, kuzungumza hadharani na kutoa misimamo tofauti.

Wakati Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF akiitisha mkutano wa waandishi wa habari Dar es Salaam jana na kusema chama chake hakipo tayari kuona uchaguzi unarudiwa, Dk Ali Mohamed Shein wa CCM amewataka wafuasi wa chama hicho kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio.

Akihutubia mkutano maalumu wa CCM wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, uliofanyika Viwanja vya Maisara Suleiman, mjini hapa, Dk Shein amewataka wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio pindi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itakapotangaza tarehe.

Rais huyo wa Zanzibar alisema jana kwamba huo ndiyo msimamo wa chama chake na hakijatafuna maneno tangu ZEC ilipotangaza uamuzi wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Alirudia kauli yake aliyowahi kuitoa hivi karibuni kwamba yeye ni Rais halali wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba na kama yupo asiyeridhika aende mahakamani ili apate tafsiri sahihi ya kisheria.

Alieleza furaha yake ya kufanyika kwa mkutano huo katika viwanja hivyo ambavyo muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Mzee Abeid Amani Karume alitoa tamko la kufuta ubepari, kupinga dhulma, kutaifisha ardhi na kufuta vyama vyote vya siasa, baada ya kupigiwa mizinga Machi 8, 1964.

Mkutano huo pia ulikuwa ni kilele cha matembezi ya Vijana wa CCM (UVCCM), yaliyoanza Januari 9 katika Jimbo la Kitope, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja.

Viongozi mbalimbali wa CCM akiwamo Kaimu Katibu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka ambaye alisema matembezi hayo ni kielelezo cha utayari wa vijana katika kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Kuhusu mazungumzo ya kukwamua hali ya mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar, Shaka alisema: “leo Januari 11 tunaomba tuanze kuitumia ile kaulimbiu ya Rais wa Muungano ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa kuamua vile vikao vya Ikulu sasa basi au tutahesabu kuwa ni ufujaji wa mali ya umma.” Wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ambaye alisema: “Kuna njama zinafanywa ili vyama vidogo visishiriki uchaguzi lakini sisi tunasema hata ikiwa CCM peke yake tutashiriki uchaguzi.” Alisema hakuna haja tena ya kuendelea na mazungumzo hayo. “…Tujiandae na uchaguzi wa marudio.

Nasikia wenzetu wamejiandaa siku ikitangazwa tarehe ya uchaguzi watatumia nguvu ya umma, sisi tunawakaribisha wafanye hivyo na matokeo yake watakuja kuyaona.” Kwa upande wake, Samia aliwaomba vijana wadumishe umoja na mshikamano.

Vijana hao wa CCM waliomba uongozi wa chama hicho kumvua uanachama Rais mstaafu, Amani Karume kwa madai kuwa hana masilahi na chama, yeye na familia yake. “Kwa kauli moja umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi tunataka avuliwe uanachama na afukuzwe mara moja Amani Abeid Karume,” alisema mmoja viongozi wa umoja huo.

MTANZANIA

Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Leticia Nyerere, amefariki dunia.

Leticia,  alifariki juzi usiku katika Hospitali ya Doctors Community iliyopo Maryland nchini Marekani alikokuwa  amelazwa tangu mwishoni mwa mwaka jana akipatiwa matibabu dhidi ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Msemaji wa familia ya Mageni Msobi, John Shibuda alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.

Shibuda, alisema hata hivyo taarifa kamili kuhusu maandalizi ya mazishi, itatolewa baada ya vikao vya familia kufanyika.

“Ni kweli amefariki dunia, sisi kama familia tutakaa na kujadiliana mipango ya kuusafirisha mwili wa marehemu kuja nyumbani kwa ajili ya mazishi,” alisema Shibuda.

Wakati mwanasiasa huyo ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) alipokuwa akipata matibabu nchini Marekani, zilizushwa taarifa za  kifo chake.

Familia yake ilikanusha taarifa hizo na kueleza kuwa Leticia alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na hali yake ilikuwa mbaya.

Leticia aliolewa na mtoto wa Hayati Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere mwaka 1996 na baadae walitengana, ingawa walifanikiwa kupata watoto watatu.

Enzi ya uhai wake, Leticia alichukua uraia wa Marekani na kuishi kwa muda mrefu nchini humo, kabla ya kurejea nchini ambapo mwaka 2010 aliteuliwa kuwa mbunge wa viti maalumu (Chadema) kwa miaka mitano.

MTANZANIA

Hali ya kisiasa visiwani Zanzibar sasa ipo gizani baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kutangaza kuwa suala la kurudiwa uchaguzi si suluhisho na haikubaliki kwani hakuna hoja wala msingi wa kikatiba kufanya hivyo.

Pamoja na hali hiyo, amesema anashangazwa na wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, hasa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, kudai kuwa ameagizwa na Rais Dk. John Magufuli kurudia uchaguzi jambo ambalo alidai si kweli.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema moja ya makubaliano ya vikao vya kamati ni pamoja na kutoa taarifa ya pamoja, lakini Balozi Seif na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein wamekiuka na kuanza kusema hadharani mambo ambayo hayajadiliwa katika vikao hivyo.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema pamoja na hali hiyo hadi sasa wamefanikiwa kufanya vikao vinane ambapo cha kwanza kilifanyika Novemba 9, mwaka jana baada ya yeye kumwandikia barua Dk. Shein kuhusu haja ya kukutana na kujadiliana hasa baada ya kufutwa kwa uchaguzi.

Maalim Seif alisema kwamba katika vikao vyote walivyokutana bado Dk. Shein na Balozi Seif wamekuwa waking’ang’ania suala la kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo, huku wakimtetea kwa nguvu zote Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Alisema lakini wakati wote yeye amekuwa akisisitiza haja ya kuheshimu maamuzi ya wananchi waliyoyafanya Oktoba 25, mwaka jana katika uchaguzi ambao waangalizi wa ndani na nje na hata Mwenyekiti wa ZEC, walisema ulikuwa huru wa haki na ulifanyika kwa amani na utulivu.

“Rais John Magufuli amefanya kazi kubwa ya kututia moyo ili tukamilishe mazungumzo kwa ufanisi na kwa kuzingatia matakwa ya katiba na sheria. Alikutana na mimi na baadaye Dk. Shein.

“Hata hivyo inasikitisha kwamba hata yeye Rais Magufuli hakuachwa kufitinishwa na wananchi wa Zanzibar, hasa pale Balozi Seif Ali Iddi alipodai hadharani kwamba eti Rais Magufuli katutaka turudi Zanzibar tukamilishe taratibu za kurudia uchaguzi jambo ambalo si kweli na Magufuli hakuniambia nilipokutana naye katika mazungumzo yetu,” alisema Maalim Seif

Alisema kutokana na kutofikiwa mwafaka wa pamoja, walikubaliana kuandaa taarifa ya pamoja ambayo ilielezwa kwamba ingeandaliwa na katibu wa vikao hivyo, lakini sasa ni zaidi ya wiki mbili hakuna kikao kilichoitishwa.

Maalim Seif alisema alilazimika kuandika barua ya kuhimiza kikao cha kupokea taarifa hiyo na kuipitisha, lakini bado Dk. Shein anadai wanahitaji muda.

“Ni wazi kwamba Dk. Ali Mohamed Shein hakuwa na nia njema katika mazungumzo haya na amepoteza sifa ya kuongoza vikao hivyo,” alisema.

Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CUF, alisema hivi sasa kuna kile alichodai ni njama za wazi zinazofanywa kwa makusudi na Dk. Shein ya kukwepa kwa makusudi kuitisha kikao cha kupokea taarifa za mazungumzo hayo.

Alisema lengo ni kuhakikisha wanaishinikiza ZEC itangaze tarehe ya uchaguzi wa marudio ili baadaye itolewe hoja kwamba suala hilo limeshaamuliwa.

“Tunazo taarifa za uhakika kwamba ZEC imetakiwa kukutana Januari 14, mwaka huu kwa lengo la kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio ambao unatajwa kuwa umepangwa ufanyike Februari 28, mwaka huu. Taarifa hizo zinaeleza lengo la hatua hiyo ni kukwamisha juhudi zinazofanywa na Rais Dk. Magufuli za kutaka kuona ufumbuzi wa haki na unaozingatia matakwa ya kikatiba na kisheria unapatikana.

“Na tukiruhusu hatua hiyo, maana yake ni kuruhusu kikundi cha watu wachache wanaotumia nafasi zao kujifaidisha kibinafsi na bila kujali masilahi mapana ya nchi na watu wake na wasiojali amani na utulivu wa nchi kuitumbukiza katika balaa kubwa sana,” alisema.

Maalim Seif alisema wananchi wa Zanzibar wako taabani na wamekumbwa na fadhaa baada ya kushuhudia maamuzi yao waliyoyafanya Oktoba 25, mwaka jana kupitia uchaguzi huru na wa haki yakiwa yanakanyagwa.

Alisema wananchi wamesubiri kiasi cha kutosha kwa sababu wao viongozi wanajali amani ya nchi ambapo aliwaomba wawe na subira na sasa umefika wakati uvumilivu na subira zao vinafikia kikomo kwa kuhitaji kuona subira zao zinazaa haki.

“Ni vyema tukaweka wazi hapa kwamba kurudiwa kwa uchaguzi si suluhisho na hakukubaliki, kwani hakuna hoja wala msingi wa kikatiba na kisheria wa uchaguzi kurudiwa,” alisema.

Maalim Seif alisema kutokana na hujuma zilizofanywa katika uchaguzi wa Zanzibar mgogoro haukuwa wa lazima na unaweza kutatuliwa kwa haraka kama utakuwapo utashi na utayari wa dhati wa kisiasa na wa kiungozi ambao utazingatia masilahi mapana na endelevu ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kutokana na hali hiyo, ili kulinda misingi ya Katiba ya Zanzibar inayopelekeza utaratibu wa ZEC kufanya maamuzi kama inavyoelekezwa na kifungu cha 119 (1) na (10) ili kujenga uhalali na heshima ya tume hiyo kutekeleza kazi zake, ni lazima mwenyekiti wake Jecha akae pembeni kwa kujiuzulu au kusimamishwa kwani amefanya makosa makubwa.

 MTANZANIA

Rais Dk. John Magufuli, jana amemtembelea na kumpa pole Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye amelazwa katika Taasisi ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es salaam.

Sumaye amelazwa katika taasisi hiyo siku nne zilizopita kwa matibabu ya moyo na madaktari wanaomtibu wamemhakikishia Rais Magufuli kuwa anaendelea vizuri ikilinganishwa na wakati alipofikishwa katika taasisi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Gerson Msingwa, ilieleza kuwa pamoja na kumpa pole, Rais Magufuli pia amemwombea kwa Mwenyezi Mungu apone haraka ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kila siku.

Akizungumza mara baada ya kuonana na Rais, Waziri Mkuu mstaafu Sumaye amemshukuru Rais Magufuli kwa kwenda kumwona na kueleza kuwa kitendo hicho kimeonesha jinsi alivyo na upendo wa dhati na anavyowajali watu wake.

Kuhusu hali yake, Sumaye ambaye mwaka jana alitoka CCM na kujiunga na upinzani, alisema anaendelea vizuri, anapata matibabu mazuri na kwamba kwa kuwa hali yake ni nzuri anatarajia kuruhusiwa kuondoka hospitali hapo baada ya muda mfupi.

NIPASHE

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina, ametoa saa 48 kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, kujieleza kufuatia mkoa wake kukithiri kwa uchafu.

Akizungumza katika majumuisho ya ziara yake ya siku mbili jijini Mwanza, Mpina alisema jiji hilo ni chafu kutokana na uzembe wa watendaji  wa serikali kushindwa kutimiza wajibu waliopewa.

“Kufuatia kazi hii ya kuangalia mazingira, Mulongo anatakiwa kutoa maelezo ndani ya saa 48 kwa nini Mwanza imekithiri kwa uchafu unaochangiwa na watendaji na siyo wananchi.

Nimepita katika Soko la Kimataifa la Mwaloni Kirumba, hali imekithiri uchafu pamoja na machinjio ya jiji hilo vinatia hofu kubwa kufuatia wanaohusika kushindwa kutunza mazingira na kuuachia uchafu wote unaozalishwa hapo kuelekea ndani ya jamii, mitoni na ziwani na hivyo kuzua hofu ya wananchi kupata maradhi,” alisema Waziri Mpina.

Mpina alisema Mulongo lazima atoe maelezo ya kina kwa kuwa yeye ndiye kiongozi wa mkoa huo na ameshindwa kuwasimamia watendaji walio chini yake na kusababisha uharibifu wa mazingira na kuuendelea kuwapo kwa ugonjwa wa kipindupindu mkoani Mwanza.

NIPASHE

Wakulima wa pamba wilayani Kishapu, Shinyanga, wameitupia lawama serikali kwa kuchelewa kuunda mapema bodi ya zao hilo.

Wamedai kuwa hali hiyo imesababisha wakulima wengi wilayani hapa kuuziwa mbegu zilizooza kwa ajili ya msimu kwa kilimo wa mwaka 2015/16.

Wakulima hao wamedai kuwa licha ya kujinunulia mbegu hizo mapema na kuanza kupanda kwa mujibu wa kanuni za kilimo bora cha zao hilo, wamejikuta mbegu hizo hazioti pamoja na kupanda wakati wa mvua za vuli kwa kuzingatia kalenda ya kilimo cha pamba.

Boniface Butondo,  mkulima mashuhuri katika kata ya Lagana,  alisema jana kuwa hali hiyo imesababishwa na serikali kwa kutotekeleza uundwaji wa Bodi ya Pamba kusimamia zao hilo.

Butondo ambaye pia ni diwani wa kata ya Lagana (CCM), alisema  kampuni zilipewa jukumu la kugawa mbegu kwa wakulima, zilitoa mbegu zisizo na ubora kutokana na kutokuwepo kwa Bodi ya Pamba ambayo husumamia kazi hiyo.

Alisema hali hiyo imesababishwa na serikali baada ya kuvunja bodi iliyokuwepo na hadi sasa hakuna bodi iliyoundwa.

Butondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, alisema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wakulima kupitia kwa madiwani wao wakidai mbegu hizo kutoota.

Alisema taarifa za wataalamu wa halmshauri hiyo zinaonyesha kuwa asilimia 30 ya wakulima wa pamba wilayani Kishapu hawajaotesha pamba yao licha ya kuzitumia vyema mvua za vuli ambazo kwa mujibu kanuni za kilimo cha pamba ndizo za kupandia.

“Ukweli serikali kwa kutotekeleza uundwaji waBodi ya pamba sasa wakulima nikiwemo mimi ambaye nimelima hekta 50 za pamba bado hazija ota na asilimia 30 ya wakulima hawajaotesha vyema…..hii hi uzembe wa serikali baada ya kuvunja bodi ya pamba lakini hadi sasa imekaa kimya na badala yake kuna watumishi tu wa bodi ambao wako maofisini na hawasimamii kikamilifu zao hili”Alisema Butondo.

Aliongeza kusema kuwa,”Mimihapa nipo shambani hekta zangu 50 natumbua macho asilimia kubwa hazijaota na siyo mkulima pekee yangu hali hii ni takribani asilimia 30 ya wakulima katika halmshauri yetu ya Kishapu hiki ni kilio kikubwa kwa mkulima wa pamba”alisema Butondo.

Mwenyekiti huyo alisema kupitia kikao cha kwanza cha Baraza la madiwani, walitoa kilio kwa Mkuu wa Milaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Kishapu, wakipaza sauti juu ya kuwepo kwa hali hiyo.

Kutokana na hali hiyo uongozi wa halmashauri hiyo umempatia taarifa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga, kumwarifu pamja na mambo mengine tatizo la njaa ndani ya wilaya ili hatua zichukuliwe.

NIPASHE

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amewavisha kitanzi watendaji wa elimu walioamua mambo mbalimbali kwa shinikizo la kisiasa, kwa kuwapa muda wa kuyapitia upya ili kuyarekebisha yafuate weledi na taaluma.

Tangu mwaka 2013, wadau wa elimu wamekuwa wakilalamikia masuala ya kisiasa kuingizwa katika elimu na kusababisha kushushwa kwa viwango vya ufaulu na kuanzishwa kwa shule na vyuo visivyo na sifa.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Prof. Ndalichako alisema taasisi zote zimeanzishwa kwa sheria na hakuna mahali popote panapowataka viongozi wake kutumia maoni ya wanasiasa kufanya uamuzi.

“Taasisi zote zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Sitaruhusu siasa iingie kwenye taaluma kwa namna yoyote ile na kwa nafasi yangu kama wazirimkazi yangu si kutoa maagizo fanya hivi, anya vile’.

“Naamini hizi taasisi zina wataalamu wenye  weledi, kazi yao ni kufanya vitu vyenye masilahi kwa taifa. Labda niseme kwa nafasi yangu sitaruhusu mtu afanye uamuzi kwa msukumo wa kisiasa,  kwanza siasa anaipata kwa nani?

“Wakati mwingine tunasingizia kuwa watu wanatuingiia. Atakuingilia  vipi wakati wewe ndiwe una utalamu na isitoshe hizi taasisi zote zimeanzishwa kwa sheria na zina taratibu  zinazoziongoza kufanya uamuzi. Hakuna sehemu inasema uchukue maoni ya wanasiasa kufanya uamuzi wako.

“Lakini kama mtu ameamua kufuata siasa ni hiari yake. Sheria  inataka weledi ufuatwe na siasa kwenye elimu haiwezi kuwa na nafasi. Kama changamoto zipo, zije tuzifanyie kazi, tusikimbie tatizo kwa sababu itakuwa haisaidii.

“Mimi nawapa changamoto wenyewe (watendaji wa elimu), kama walikuwa wamefanya uamuzi kwa shinikizo la kisiasa, sasa warudi waangalie weledi, wajitathimini na kuangalia taaluma zao.  Kama ni madaktari waangalie ili mtu awe daktari viwango vyake ni vipi, mainjinia (wahandisi) bora wanatakiwa waweje na vitu kama hivyo.

“Nataka kuwarudishia wao wenyewe na nimewaambia wajitizame upya. Hata TCU (Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania) niliwaambia waangalie upya vigezo vyao. Sasa kama kulikuwa na siasa nimewapa fursa ya kujirekebisha,” alisema Prof. Ndalichako.

Aliongeza kwamba: “Nimeaambia tukisema ni hapa wote tusimame hapa hakuna kuyumba na tutaelimisha Watanzania kwa nini tunafanya hivyo na najua tutakuwa na vigezo vinavyoeleweka.”

Aliwataka wananchi pia kutoingilia mambo yanayohusu taaluma zingine kwa kuwa kwa baadhi ya maeneo, kelele zao zinafanya baadhi ya wataalamu kufanya uamuzi usio sahihi.

Kuhusu madaraja na uhalali wake, Prof. Ndalichako alisema maelezo yaliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk, Charles Msonde), alipotembelea wiki iliyopita hakuyaelewa na kuona si lazima mtu aseme mezani kila kitu.

“Watakapoleta maelezo yao Alhamisi (keshikutwa) ndipo nitaona kama ni kitu kizuri au kibaya na kama unaona pale niliwataka  wasitetereke kwenye utendaji.

“Tukipata sababu zao tutaangalia kulingana na sababu zilizotolewa nini kitafanyanyika. Mpaka sasa hatujajua, maelezo yao ndiyo yatatuambia,” alisema.

Mbali na mambo hayo, alisema licha upangaji wa madaraja ya ufaulu kwa kuangalia wastani wa alama (GPA), ambao wananchi wanaulalamikia, Necta imefanya vizuri kwenye maeneo mengi ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya utungaji mitihani, kuboresha mifumo ya utendaji kazi ya kielektroniki na kuanza kutoa vyeti mbadala kwa wahitimu ambao vyeti vyao vina picha pale vinavyopotea.

“Na kwa wale vyeti visivyokuwa na picha, bado wameendelea kutotoa vyeti mbadala. Badala  yake wanatoa ‘statement of results’ (karatasi maalumu ya matokeo) kwa sababu kwenye mambo ya vyeti kuna ‘umafia’ sana. Watu wanabadilishana vyeti na mambo kibao yapo huku,” alisema.

Vurumai kwenye mfumo wa elimu ilianza baada ya matokeo ya kitado cha nne ya mwaka 2012 kufutwa kutokana na ripoti ya Tume ya Profesa Sifuni Mchome, ambaye baada ya ripoti yake, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya kabla ya kuhamishwa na Rais John Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa wizara ya Sheria na Katiba, baada ya kumteua Prof. Ndalichako kuongoza wizara hiyo.

Matokeo ya awali mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2012, yalionyesha kuwa watahiniwa waliopata kati ya daraja  kwanza mpaka la tatu ni  23,520 sawa na asilimia 6.4, daraja la nne watahiniwa  103,327 (asilimia   28.1) huku waliopata sifuri wakiwa  240,909 (asilimia  65.5).

Baada ya ripoti ya Prof Mchome kutaka matokeo hayo yafutwe na kupangwa upya, waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 35,349 (asilimia  9.54), daraja la nne 124,260 (asilimia 33.54) na waliopata sifuri wakawa 210,846 sawa na asilimia 56.92.

Wizara pia ilibadilisha utunuku wa ufaulu na kuanza kutumia GPA, badala ya jumla ya alama (division) iliyokuwa imezoeleka.

Mbali na uamuzi huo, wizara pia ilishusha alama za ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita ambapo sasa  A inaanzia 75 hadi 100,  B+ (60 hadi 74) B (50 hadi 59), C (40 hadi 49), D (30-hadi 39), E (20 hadi 29) na  F ni kuanzia 0 mpaka 19.

Alama zilizokuwa zikitumiwa awali kwa kidato cha nne ni  A (80 hadi 100),  B (65 hadi 79) C (50 hadi 64), D (39 hadi 49) na  F kutoka 0 hadi 34 huku kidato cha sita ikiwa A (80 hadi 100), B (75  hadi 79),  C (65 hadi 74),  D (55 hadi 64) E (45 hadi 54), S (40 hado 44) na F kutoka 0 hadi 39.

HABARILEO

Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imesema iko kwenye hatua nzuri za kuanzisha mradi wa uzalishaji dawa na vifaa tiba nchini kwa ubia na sekta binafsi, lengo likiwa kupunguza tatizo la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Mwanakunu alisema zabuni ya kumpata mtaalamu mshauri imekwishatangazwa na inategemea kukamilika mwezi huu.

Alisema, kwa sasa Bohari huagiza kutoka nje ya nchi dawa na vifaa tiba takribani asilimia 80 kutokana na uchache na uwezo mdogo wa viwanda vya ndani vya kuzalisha dawa na vifaa tiba.

Bwanakunu alisema, hali hiyo huilazimu MSD kuagiza bidhaa zake kwa wingi kukidhi mahitaji ya muda mrefu na hivyo kulazimika kuwa na sehemu kubwa ya kuhifadhia bidhaa hizo.

Akizungumzia uwekaji nembo kwenye dawa za serikali, Bwanakunu alisema katika mwaka wa fedha 2013/ 2014, MSD ilianza kuweka nembo ya GOT ikimaanisha Government of Tanzania (Serikali ya Tanzania).

Alisema, nembo hiyo imewekwa kwenye vidonge, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara, kudhibiti kupelekwa kwenye maduka binafsi ya dawa, badala ya kutumiwa na walengwa ambao wanatibiwa katika hospitali zinazosambaziwa dawa na MSD.

“Awali, MSD ilikuwa ikiweka nembo ya MSD katika vifungashio tu, ambapo ilikuwa ni rahisi dawa hizo kuhujumiwa na kwenda kusikostahili. Kwa kuweka nembo hiyo ya GOT pamoja na MSD katika dawa, ni hatua mojawapo itakayosaidia kupunguza ama kudhibiti kabisa tatizo la wizi wa dawa za serikali,” Bwanakunu alisema.

Aliweka wazi kuwa hadi sasa asilimia 80 ya bidhaa zimekwishawekewa nembo ya GOT na kwamba wazabuni wengine wote wanaopata zabuni za kupeleka dawa kwenye bohari hiyo wanaelekezwa kuzingatia utaratibu huo wa kuweka nembo ya GOT na MSD.

“Kufikia Juni 2016 nembo ya MSD na GOT zitakuwa zimewekwa kwenye bidhaa zote,” alisema katika taarifa yake kwa gazeti hili.

Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.

Tupia Comments