MWANANCHI
Jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa limeibuka bungeni baada ya mbunge mmoja kuiuliza Serikali kuwa haioni haja ya kubadili sheria ili viongozi wa zamani wa kitaifa wasipewe stahiki zao iwapo wanahama vyama baada ya kutoka madarakani.
Mbunge huyo wa Dimani, Hafidh Ali Tahir alihoji kama Serikali haioni kuwa iko haja ya kufanyia marekebisho sheria ya kuwapa stahiki zao baadhi ya mawaziri wakuu wastaafu waliohama vyama vyao kwa kuwa zilitokana na nguvu za vyama walivyovihama.
“Msingi wa swali langu ulikuwa ni kuangalia suala la ulafi wa madaraka na hii si kwa mawaziri wakuu wastaafu pekee, bali hata huko upande wa upinzani kuna mbunge aliwahi kuwa katibu mkuu wa wizara mbalimbali, naomba ufafanuzi,” alisema Hafidh huku akimtaja Lowassa kuwa aligombea urais kwa tiketi ya upinzani baada ya kuihama CCM.
Hata hivyo, Serikali ilimtetea Lowassa kuwa uamuzi wake wa kugombea urais baada ya kuihama CCM ulikuwa halali na ndiyo maana bado anastahili kulipwa posho kama stahiki zake. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angela Kairuki alijibu kuwa kitendo cha Lowassa kugombea urais ni haki yake ya msingi kama ilivyo kwa Watanzania wengine.
“Haki ya kujiunga na chama chochote cha siasa au kujihusisha na masuala ya siasa ni ya kikatiba, na kwa kuwa haki hizi haziwezi kuzuiwa au kuingiliwa, ni wazi kuwa suala la kufanyia marekebisho sheria ya mafao kwa viongozi wa kitaifa waliostaafu, bado haliwezekani,” alisema Kairuki. Alisema kuwazuia mawaziri wakuu wa zamani au viongozi wengine wastaafu wa kitaifa kujiunga na chama chochote cha siasa, itakuwa kinyume na Katiba ya nchi.
Waziri Kairuki alisema Lowasa hajapoteza stahiki zake isipokuwa kama angepata nafasi hiyo, kungekuwa na uamuzi mwingine.
Hata hivyo, hoja hiyo ilionekana kupigiwa kelele na wabunge wengi, akiwamo kiongozi wa kambi ya upinzani, Freeman Mbowe ambaye alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watumishi wanaotumia mwamvuli wa CCM kuwanyima haki wanasiasa wa upinzani.
Lakini Waziri Kairuki alisema kama watumishi wataingilia masuala ya kisiasa, watakuwa wanakiuka sheria. Hata hivyo, alisema wanapokuwa kwenye utumishi hutakiwa kutekeleza Ilani ya CCM, hivyo hawana budi kufanya hivyo.
MWANANCHI
Mahakama Kuu imewahukumu kifungo cha maisha jela, watu wawili baada ya kupatikana na hatia katika kesi mbili tofauti za kusafirisha dawa za kulevya zenye thamani ya Sh289.2 milioni.
Washtakiwa hao waliohukumiwa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari ni Hamis Suya, mkazi wa mkoa wa Tanga na Josephine Mumbi Waithera, raia wa Kenya.
Josephine alikuwa akishtakiwa kwa kusafirisha gramu 3,249.82 za dawa hizo aina ya heroini zenye thamani ya Sh146.2 milioni kwenda Vienna, Austria kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia) wakati Suya alikamatwa akisafirisha gramu 3,191.3 za heroini zenye thamani ya Sh143 milioni kwenda jijini Arusha kwa Basi la Happy Nation.
Akitoa hukumu dhidi ya Suya, Jaji Sumari alisema upande wa mashtaka umeithibitishia Mahakama bila kuacha shaka kuwa alikutwa na dawa hizo.
Alisema hakuna ubishi kuwa tembe 249 za heroini zikiwa ndani ya begi kwenye basi hilo lililokuwa likisafiri kati ya Dar es Salaam na Arusha Novemba 27, 2012 zilikuwa za mshtakiwa huyo.
“Hoja hapa ilikuwa nani ni mmiliki wa begi lile kati ya washtakiwa hawa watatu, yaani Mussa Mgonja, Suya na Abdulaziz Makuka, lakini kulikuwa hakuna ubishi begi la dawa zile lilikutwa ndani ya basi,” alisema Jaji Sumari.
Alisema kitendawili hicho kiliteguliwa na maelezo ya Suya aliyoandika polisi na kukiri kosa hilo na kuwa aliyatoa kwa hiari yake bila kulazimishwa.
Alisema pamoja na utetezi wa wakili Diana Solomon kuwa mshtakiwa huyo ni mgonjwa na anategemewa na familia, kifungo cha kosa hilo ni kimoja tu, nacho ni jela maisha na hakuna adhabu mbadala.
Jaji Sumari aliwaachia huru washtakiwa Mgonja na Makuka baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha jinsi walivyotenda kosa hilo. Kuhusu kesi ya Josephine, Jaji alisema: “Anadai (Josephine) hakujua unga huo ulikuwa ni dawa za kulevya na kwamba alibeba unga wa dhahabu, bado hakuna ubishi unga huo anaodai ni wa dhahabu umethibitika ni dawa za kulevya.”
Jaji Sumari alisema hana shaka yoyote ya kutoamini hadithi iliyopo katika maelezo yake hayo namna begi hilo lilivyoingia mikononi mwake jijini Arusha, hivyo yeye ndiye mhusika wa dawa hizo.
Kupitia kwa wakili Raplh Njau aliyekuwa akimtetea, mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu kwa madai kuwa ni mzazi wa watoto wanne na anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari. Hata hivyo, Jaj
NIPASHE
Mahama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema itaendelea kusikiliza ushahidi wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Gwajima anakabiliwa na tuhuma za kutoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwamba ni mtoto, hana akili na mpuuzi. Anadaiwa kutoa maneno hayo.
Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa ushahidi huo jana lakini iliahirishwa baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, anayeendesha kesi hiyo kuwa mgonjwa.
Kimaro alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha, anayesikiliza kesi hiyo.
Wakili wa utetezi Peter Kibatala, alidai kuwa hana pingamizi na maombi ya Jamhuri.
Hakimu Mkeha alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Februari 24, mwaka huu na dhamana ya mshtakiwa inaendelea.
Katika kesi ya msingi, Askofu Gwajima anadaiwa kuwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka jana, katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam, alitoa lugha ya matusi kwamba “mimi Askofu Gwajima nasema Askofu Pengo ni mpuuzi mmoja yule, mjinga mmoja, amekula nini yule, sijui amekula nini yule mtoto hana akili yule”.
Alidai kuwa Askofu Gwajima alitoa maneno hayo ya kufadhaisha dhidi ya Kardinali Pengo na kwamba yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
NIPASHE
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, amewaagiza viongozi kuhakikisha wale wote waliohusika na wizi wa fedha za wakulima kufikishwa mahakamani mara moja.
Alitoa agizo hilo bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, aliyehoji kuhusiana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013 iliyoelezea upotevu wa Sh. bilioni 28 za wakulima wa zao la tumbaku mkoani Tabora.
Nchemba alisema hiyo ripoti anaifahamu na kuagiza wale wote waliohusika katika kuwaibia wakulima hao kuchukuliwa hatua.
Alisema suala hilo halipo kwenye tumbaku tu, kwani kuna maeneo mengine ambayo yana changamoto hiyo ya wakulima kuibiwa fedha zao na kuahidi kuwashughulikia wote waliohusika baada ya Bunge kumalizika.
Alisema serikali imepanga kupitia makato yote yanayokatwa kwa wakulima na ndani ya siku mbili atatoa tamko juu ya suala hilo.
Nchemba alisema Rais John Magufuli ameshaonyesha kukerwa na tozo nyingi za makato kwa wakulima, hali ambayo inawafanya wakose maendeleo, hivyo atalishughulikia suala hilo kwa wakati.
NIPASHE
Serikali inapanga kujenga vyuo vya uvuvi katika mikoa yote ambayo ina bahari ili kusaidia wananchi kupata ujuzi kuhusiana na shughuli za uvuvi na kujipatia kipato.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha,alisema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali, aliyetaka kujua kama serikali haioni umuhimu wa kujenga chuo mkoani Lindi ambako kuna Bahari ya Hindi ili kuwaongezea vijana hao ujuzi na kupata ajira.
Ole Nasha alisema Rais John Magufuli, ameonyesha nia ya dhati ya kutaka kuwasaidia wananchi na wizara yake inatambua umuhimu wa kuwafundisha vijana mbinu sahihi za kufanya shughuli za uvuvi, kilimo na ufugaji na ndiyo maana kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi imeanzisha Chuo cha Uvuvi Mikindani kwa lengo la kusogeza huduma ya mafunzo ya uvuvi kwa wananchi wakiwamo vijana walioko ukanda wa kusini mwa Tanzania ikiwemo Lindi.
HABARILEO
Daraja la mto Koga lililopo mpakani mwa mikoa ya Katavi na Tabora, limefurika maji ya mvua na kusababisha vifo vya watu sita, ambao wamesombwa na maji.
Pia mafuriko hayo yamesababisha foleni ndefu ya magari katika eneo la mto huo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka mjini Mpanda jana jioni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahri Kidavashari alisema watu hao waliosombwa na maji na miili yao haijaonekana, hadi sasa ni wanawake wawili na watoto wanne.
Alisema watu hao wamefikwa na umauti baada ya gari aina ya Toyota Pick Up yenye namba za usajili T597 BTC, kusombwa na maji wakati likijaribu kuvuka Mto Koga uliokuwa umefurika maji.
Kufurika maji kwa daraja la Mto Koga, kumesababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara kati ya miji ya Mpanda mkoani Katavi na Sikonge mkoani Tabora, na kusababisha kero kubwa kwa mamia ya abiria.
Inadaiwa kuanzia juzi zaidi ya 100 yalikuwa yamekwama huku idadi kubwa ya abiria wakikwama pia katika eneo hilo.
Walieleza kuwa wamesubiri kwa muda muda mrefu maji yapungue.
Miongoni mwa waathirika hao ni wanawake na watoto, wanaotumia miundombinu kwa ajili ya kwenda kliniki na shuleni, wamelazimika kulala eneo la mto huo kusubiri maji yapungue.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, ajali hiyo ilitokea juzi saa 12 jioni baada ya gari hilo lililokuwa likitokea Tabora kwenda mjini Mpanda kufika katika eneo hilo la Mto Koga na kukuta foleni ya magari yakisubiri kuvuka.
HABARILEO
Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) imempongeza Rais John Magufuli kwa kushirikiana na jumuiya hiyo, hivyo kufanikisha serikali kukusanya kiasi cha Sh trilioni 1.4.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Johnson Minja wakati akizindua tawi la JWT Mkoa wa Pwani.
Alieleza uundwaji wa kamati ya wafanyabiashara, umesaidia kupatikana kwa kiasi hicho kwa muda mfupi.
Minja alisema kamati hiyo ilisaidia kuonesha jinsi baadhi ya watendaji wa serikali walikuwa wakishirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu, kuikosesha mapato serikali.
“Tunamshukuru Dakta Magufuli kwa kuonesha ushirikiano pamoja na sisi, kwani ameamini kuwa nchi inaweza kujiletea maendeleo kwa kushirikiana na wafanyabiashara ambao ni sekta binafsi na matokeo ya ushirikiano yamezaa matunda,” alisema Minja.
Alisema kipindi cha nyuma, fedha nyingi za kodi zilikuwa zikiingia kwenye mifuko ya watendaji wasiokuwa waaminifu, badala ya kwenda serikalini.
Alisema mapato yaliyokuwa yakienda serikalini, yalikuwa kidogo.
“Wafanyabiashara si kwamba hawataki kulipa kodi, tatizo ni kwamba kodi nyingi zilikuwa za usumbufu na pia watendaji wa mamlaka za ukusanyaji, walikuwa wakijipatia fedha kwa maslahi binafsi, lakini Dakta Magufuli ameliona hilo na amewashughulikia wale waliokwepa kodi na kuwashirikisha wafanyabiashara,” alisema Minja.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani, Abdalla Ndauka alisema lengo la kuanzishwa jumuiya hiyo ni kuwaunganisha wafanyabiashara na kuwa na sauti moja ili kukabili changamoto zinazowakabili.
Ndauka alisema moja ya changamoto zao ni kuwa na kodi nyingi huku nyingine zikiwa siyo sahihi na nyingine zimekuwa ni kero, lakini pia lengo ni kuongeza walipa kodi kwa usajili wa wafanyabiashara ili wawe rasmi.
HABARILEO
Wafanyakazi saba kati ya wanane wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) waliotuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,019 na magari 2,019 kutoka bandarini ambao walitoroka, wamepatikana na tayari wanaendelea kuhojiwa na polisi juu ya tuhuma hizo.
Watumishi hao ni kati ya watuhumiwa 15 wa TPA waliotangazwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuwa wameshiriki kuondosha makontena na magari hayo kutoka katika bandari kavu saba bila kulipa ushuru wa Bandari.
Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi aliliambia gazeti hili jana kuwa mfanyakazi mmoja kati ya hao wanane, hajapatikana; na anaendelea kusakwa na polisi ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
“Wote walishapatikana kasoro mtumishi mmoja, Happygod Naftali, ambaye huyu alishaacha kazi siku nyingi baada ya viongozi kuanza kufuatilia suala hilo; lakini bado polisi wanaendelea kumsaka,” alisema Ruzangi.
Mkuu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alithibitisha watuhumiwa hao, kukamatwa na kwamba bado wanaendelea kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo.
“Ni kwamba tunaendelea na upelelezi wetu,” alisema Sirro licha ya kuwa hakutaka kutaja idadi ya wafanyakazi wa TPA ambao wamepatikana. “Kwa kweli idadi nitaitoa siku nitakapozungumza na waandishi wa habari wiki hii,” alifafanua.
Watumishi waliokuwa wanasakwa na polisi waliopatikana kwa mujibu wa Ruzangi ni Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Bonasweet Kimaina, Zainab Bwijo na Nathan Edward.
Watumishi hao wanaungana na watumishi wengine saba John Elisante, Leticia Masaro, Christina Temu, Merina Chawala, Adnan Ally, Masoud Seleman na Benadeta Sangawe waliokamatwa na kuhojiwa kuhusu sakata hilo. Watumishi hao saba, kwa mujibu wa Sirro, tayari walishapelekwa mahakamani.
“Ukiacha wale saba ambao tumeshawafikisha mahakamani, hawa wengine bado tuko nao tunaendelea kufanya upelelezi,” alieleza.
Wafanyakazi hao wanatuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,884 na magari 2,019 ambayo yalitoroshwa kutoka katika Bandari Kavu (ICD) saba bila kulipiwa ushuru wa bandari na hivyo kuipotezea Serikali mapato ya Sh bilioni 48.55.
Kuhusu mawakala 280 waliopewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo yao makao makuu ya TPA namna ya walivyohusika kulipia makontena hayo, Ruzangi alisema mamlaka yake inajipanga kutoa taarifa kamili juu ya suala hilo.
“Tunaendelea kuandaa taarifa ya kilichotokea na kilichobainika kuhusu mawakala hao, tutatoa taarifa hivi karibuni,” alisema Meneja Mawasiliano huyo.
Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, uongozi wake umeibua ufisadi wa kutisha ambao ulikuwa unafanywa Bandari ya Dar es Salaama kwa kuwashirikisha wafanyakazi wa TPA na mawakala pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Kwa mara ya kwanza upotevu wa makontena 349 uligundulika baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutinga bandarini na kubaini makontena hayo kutolewa bandari kavu bila kulipiwa kodi. Upotevu huo ulifanya vigogo wa TRA, akiwemo Kamishna Mkuu Rished Bade na makamishna wengine kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani.
Baadaye Majaliwa alibaini upotevu wa makontena 2,431 yaliyoondolewa bandari kavu bila kulipiwa ushuru wa Bandari.
Katika sakata hilo, baadhi ya mawakala wa forodha walifungiwa kufanya biashara na TPA Sakata la mwisho ni la kupotea kwa makontena 11,019 na magari 2,019, ambayo yaliondolewa kwenye ICD saba bila kulipiwa ushuru wa bandari na kuipotezea serikali mapato ya Sh bilioni 48.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyeza hapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE