Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia Uhuru aliyekuwa Mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Godfrey Gugai,Geogre Makaranha na Leonard Aloys baada ya mahakama hiyo kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo amesema kutokana na mashtaka kushindwa kuthibitishwa na Upande wa Jamhuri, mahakama imeshindwa kuwatia hatiani kwahiyo watuhumiwa wote wapo huru.
Hukumu hiyo inakuja baada ya Gugai kufikishwa mahakamani hapo, Novemba 16, 2017.
Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 382/2017 ni George Makaranga na Leonard Aloys.
Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake, wanakabiliwa na makosa 40, makosa 19 kati ya hayo ni ya kughushi, 20, ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.
Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba, 2015.
Inadaiwa mshitakiwa akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa TAKUKURU alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni, ambazo hazilingani na kipato chake cha awali na cha sasa, huku akishindwa kuzitolea maelekezo.