Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa ametoa siku saba kwa Katibu Mkuu Wizara hiyo Anthony Sanga kuhakikisha timu ya wataalamu inafika kushughulikia mgogoro wa ardhi baina ya halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na wilaya ya Nyang’wale Mkoa wa Geita.
Ametoa agizo hilo leo Jumatatu Desemba 4, 2023 wakati akizungumza na baadhi ya viongozi, maafisa, watumishi wa idara ya ardhi pamoja na wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga wakiwemo wakuu wa Wilaya na wabunge kutoka kwenye majimbo ya Mkoa wa Shinyanga.
Waziri Silaa amewataka viongozi hao kufuatia hoja iliyotolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje kuhusu mgogoro huo wa mpaka wa muda mref.
Mara baada ya kupokea hoja hiyo Waziri Silaa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha timu inayoongozwa na Mkurugenzi wa Upimaji Ramani inafika na kushughulikia changamoto hiyo na taarifa yake aipate kabla ya tarehe 14 Desemba 2023.
Katika agizo hilo pia Waziri Silaa amemtaka Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Stella Tulo kufika Mkoani Shinyanga ndani ya siku saba na kuona kazi zinazofanywa na Mabaraza hapa shinyanga.