Top Stories

Unaambiwa ujenzi wa Terminal 3 ni BILIONI 560, Mkurugenzi TIC azungumza

on

Ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kwa kuongeza ‘Terminal 3’ umekamilika kwa asilimia themanini na mbili (82%).  Ujenzi huo ulianza mwezi Juni mwaka 2013 na unatarajiwa kukamilika May 2019 ambapo gharama za kukamilisha ujenzi huo utafikia takribani  zaidi ya Bilioni 560.

Jengo hilo lina ghorofa tatu ambapo ghorofa ya kwanza ni kwa ajili ya wasafiri wanaofika, ghorofa ya pili ni kwa ajili ya wasafiri wanaoondoka na ghorofa ya tatu ni masuala ya utawala na una miundombinu ya kisasa ya kielektroniki.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga Tanzania (TAA) Richard Mayongela akizungumza mbele ya Mkurugenzi wa TIC, Mwambe  amesema Kukamilika kwa uwekezaji huo kutaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na kuchochea uwekezaji zaidi. 

Mkurugenzi Mkuu wa TAA (kati) Richard Mayongela akiwa na mgeni wake Mkurugenzi Mtendaji wa TIC  Geoffrey Mwambe (kushoto) kwa ziara ya kutembelea uwanja wa JNIA- Terminal 3

Mwambe kama mdau wa uwekezaji alifanya ziara lengo ni kuhakikisha kwamba uwekezaji huo unavutia na kuchochea wawekezaji kuja kuwekeza zaidi nchini, unatoa huduma bora kwa wasafiri wakiwemo wawekezaji, unarudisha faida kwa Serikali, Watanzania na Taifa kwa ujumla kama inavyotarajiwa.

TIC ni taasisi ya Serikali, ambayo imekuwa ikifanya juhudi za kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na hivyo kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo, kutasaidia kuongeza idadi ya wawekezaji, kutokana kutoka mataifa mbalimbali kutokana na ukweli kwamba uwepo wa miundombinu bora kunahamasisha na kuvutia zaidi wawekezaji kwani wanakuwa na uhakika wa kusafirisha malighafi kwa ajili ya viwanda na bidhaa zinazozalishwa kwenda kwenye soko la ndani na nje ya nchi kwa urahisi.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA Mayongela akimweleza jambo Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Bw. Mwambe

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mwambe amesema kukamilika kwa uwanja huo kutasaidia kuongeza tija kwenye uwekezaji kwani nchi zilizo na miundombinu bora (barabara, viwanja vya ndege, bandari) duniani ndizo zinazopata wawekezaji wengi.

Kufuatia upanuzi huo kutatokea fursa za uwekezaji ikiwemo makampuni mapya ya ndege kuanza kutua Tanzania jambo ambalo litaleta ushindani wa biashara kwenye sekta ya anga. Hali hiyo itasaidia kupunguza gharama na nauli za usafiri kwa Wananchi pia wataweza kuongeza uwezo wa kuchagua aina ya shirika la ndege ambalo wangependa kusafiri nalo.

Maeneo mengine ya uwekezaji ambayo Wazawa wanakaribishwa kuchangamkia fursa ni katika maeneo ya kuendesha usafiri wa magari madogo ‘tax’, kuendesha maegesho, kuanzisha maduka ya biashara ‘duty free’, kuendesha hoteli, kuendesha maduka ya mvinyo.

Kutokana na uwekezaji huo matarajio ya Serikali ni kuhakikisha inatoa huduma nzuri kwa wadau wakiwemo watalii, wafanya biashara na wawekezaji, inavutia zaidi wawekezaji,  inatengeneza ajira kwa Watanzania, inapata kodi na mapato kwa ajili ya kuendesha huduma za jamii na kuinua hali ya Watanzania na uchumi wa Taifa.

Mambo yanazidi kunoga, Uwanja wa Ndege Terminal 3 kukamilika mwakani

 

 

 

 

 

 

 

Soma na hizi

Tupia Comments