Miaka 60 ya ushirikiano baina ya Serikali na Tanzania na Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA,) imekuwa ya mafanikio makubwa hasa kwa JICA kuendelea kukua na kujitanua zaidi katika kusaidia katika kutoa misaada na kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na uchumi nchini kwa kushirikiana na Serikali kwa kufuata vipaumbele vya watanzania.
Hayo yameelezwa leo na Mwakilishi Mkuu wa wa JICA nchini Naofumi Yamamura wakati wa semina maalum kwa waandishi wa habari pamoja na ziara ya kutembelea baadhi ya miradi iliyofadhiliwa na JICA uki wemo mradi wa kituo cha kupooza umeme kilichopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na mradi wa daraja la juu ‘Mfugale Flyover’ lililopo Tazara jijini Dar es Salaam.
Amesema mahusiano baina ya Tanzania na Japan na Tanzania yalianza 1962 mara baada ya Uhuru wa Tanganyika na wataendelea kushiriki na kufadhili miradi mengi Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar kwa manufaa ya nchi hizo mbili ambapo watanzania 22,064 wamenufaika na programu za mafunzo zilizodhaminiwa na Serikali ya Japan huku Wajapan 1,679 wameshiriki program hizo za mafunzo na kunufaika na mambo mengi kutoka Tanzania ikiwemo utamaduni na lugha ya Kiswahili.
Aidha ameeleza ushirikiano huu uliudumu kwa miaka 60 na kutekeleza miradi mbalimbali Tanzania ikiwemo mradi wa ujenzi wa daraja la Salender 1980 utaendelea kudumu kwa manufaa ya watanzania.
Kwa upande wake Mwakilishi Mwandamizi wa (JICA,) Watanabe Hideki ameeleza kuwa kwa miaka 60 Serikali ya Japan kupitia JICA wameendelea kukuwa na kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia vipaumbele vya watanzania, huku Japan ikinufaika na mengi kutoka Tanzania ikiwemo kahawa ya Kilimanjaro Coffee, korosho na bidhaa za kilimo ambazo zinakubalika sana katika soko la Japan.
Amesema, kuanzia awamu ya kwanza ya uongozi wa Hayati. Julius K. Nyerere hadi katika awamu hii ya sita JICA inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya kijamii na maendeleo ikiwemo miradi ya ujenzi wa soko la samaki ‘Malindi Fish Market’ Zanzibar, ujenzi wa daraja la juu Gerezani, Dar es Salaam, ujenzi wa barabara mpya ya Bagamoyo ‘New Bagamoyo road’ Dar es Salaam sambamba na mradi mpya wa kuhimiza ujasiriamali na uvumbuzi kupitia Japan Project ‘NINJA na mradi wa kuhimiza usawa wa kijinsia ‘Ladies First’ mradi utakaoshirikisha sekta binafsi pamoja na mafunzo kupitia elimu na kubadilishana teknolojia.
Katika mradi wa kituo cha kupooza na kusambaza umeme kilichopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mhandisi mwandamizi wa Idara ya Usafirishaji Umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO,) Kanda ya Mashariki Gwamaka Thobias amesema, kituo hicho kilichozinduliwa mwaka 2017 kwa ufadhili wa JICA kimekuwa msaada mkubwa katika uendeshaji wa hospitali hiyo kutokana na uhakika wa nishati ya umeme kwa muda wote.
‘’Taasisi nne zinanufaika na umeme kutoka katika kituo hiki ikiwemo Taasisi ya Moyo (JKCI,) Taasisi ya Mifupa (MOI,) Muhimbili pamoja na Chuo….nishati ni ya uhakika inafika moja kwa moja na kupoozwa katika kituo hiki na upatikanaji wa nishati ni wa uhakika na muda wote.’’ Amesema.