Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hii leo inaadhimisha kumbukumbu ya miaka hamsini ya mapinduzi ambayo kwenye historia yanaonyesha yalimaliza utawala wa Kisultani visiwani humo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameongoza sherehe hizo ambazo pia zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Tanzania bara akiwemo rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wa Rais Dkt Mohamed Ghalib Bilal.
Miongoni mwa marais kutoka nchi jirani waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.
Rais Shein amewataka wananchi kuonesha umoja na mshikamano walionao katika sherehe hizo za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar zinazofanyika kwenye viwanja vya Amani Mjini Unguja.
Katika risala yake Dokta Shein ametangaza siku ya Jumatatu kuwa siku ya mapumziko kwa Zanzibar na kusema kuwa atamshauri Rais Kikwete iwe pia na kwa upande wa Tanzania Bara.