Mke wa Rais wa zamani wa Marekani Michelle Obama ametangaza uzinduzi wa kampuni yake ya vyakula na vinywaji vyenye afya ambayo ameianzisha ili kuwapa Wazazi bidhaa bora na zenye ladha nzuri kwa ajili ya Watoto wao.
Michelle Obama amezindua kampuni hiyo iitwayo “PLEZi Nutrition” ambapo bidhaa yake ya kwanza ni juisi ya matunda hususani kwa Watoto iliyo na sukari chini ya 75% kuliko wastani wa juisi za matunda zenye 100% ya sukari.
PLEZi tayari inapatikana katika baadhi ya maduka ya rejareja huku kampuni ikipanga kusambaza vitafunio na vinywaji vingi zaidi katika miaka michache ijayo ikilenga kupunguza kiwango cha sukari ili kuwatengezea Watoto mazingira ya kutotamani vitu vyenye sukari nyingi kwa ajili ya kuboresha afya yao.
Itakumbukwa Michelle Obama katika nafasi yake wakati akiwa Mke wa Rais aliongoza kampeni iitwayo “Let’s Move” ambao ni mpango unaolenga kukomesha hali ya unene wa kupindukia kwa Watoto, mafanikio ya kampeni hiyo yalikuwa makubwa kutokana na kupitishwa kwa Sheria ya Watoto nchini Marekani ambayo iliunda viwango vya lishe vya shirikisho kwa chakula cha mchana ambacho Watoto hupatiwa mashuleni.
CNN ililiripoti hapo awali kwamba Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Marekani vilisema kiwango cha unene wa kupindukia kilipungua kwa asilimia 43 miongoni mwa Watoto wadogo wenye umri wa miaka miwili hadi minne kati ya 2004 na 2012 lakini licha ya jitihada za Michelle na Wadau wengine viwango vya unene wa kupindukia kwa Watoto vimeongezeka kwa Watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 11 ishara kwamba baadhi ya juhudi chini ya utawala wa Obama huenda hazikufanya kazi vizuri.