Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema miili 13 ya watu waliofariki baada ya kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo, itaagwa Novemba 18, 2024 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Akizungumza usiku wa kuamkia leo RC Chalamila amesema shughuli ya kuaga miili hiyo itaongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa huku ndugu wa marehemu wakitaiwa kukutana katika Hospitali ya Amana saa 2 asubuhi ya Novemba 18, 2024 kwa ajili ya taratibu mbalimbali.
“Hatujasitisha zoezi la uokoaji bali kutokana na ushauri wa madaktari ni kwamba imeonelewa miili hiyo 13 iagwe kwanza wakati uokoaji ukiendelea,”
Mbali na hilo, RC Chalamila ametoa angalizo kwa watu wanaotumia mitandao ya kijamii wakidai kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia manusura wa tukio hilo.
“Nitoe rai kwamba tumekwishaanza kupata minong’ono ya baadhi ya watu kuanza kutumia tukio hili kinyume na utaratibu na sheria zilizopo za maafa kwa wote ambao wanatumia mwanya kutapeli watu kuwa na Lipa namba ambazo hazijthibitishwa ama kuwa na Lipa namba ambazo wanatumia jina la serikali kujinufaisha naomba nitoe rai kwamba wanaweza kuchukulia hatua kali za kisheria kwa sababu muda huu sio wa kujinufaisha bali wa kuwaokoa wenzetu, sisi kama Serikali na Mhe.Rais amekwisha elekeza kwamba gharama zote za msingi zibebwe na Serikali na Ofisi ya Mhe.Waziri Mkuu ndio itakayoratibu maswala yote ya gharama kuanzia majeneza hadi usafiri,” amesema Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.