Jake Paul na Mike Tyson wamefungiwa rasmi kushiriki ngumi kwa muda baada ya pambano lao lenye utata lililofanyika Jijini Dallas wikiendi iliyopita ambapo Katika pambano hilo Jake Paul alitangazwa mshindi kwa uamuzi wa point za Majaji dhidi ya Tyson mwenye umri wa miaka 58, huku akishutumiwa na Mashabiki zake kwa kumhurumia mpinzani wake aliyekuwa dhaifu mwishoni mwa pambano.
Paul, ambaye aliahidi kumuangusha Tyson kwa KO lakini hakutimiza ahadi hiyo aliomba msamaha kwa Mashabiki wake, akieleza kuwa aliona huruma kwa mpinzani wake aliyekuwa amechoka huku akisema hakuwa na nia ya kumuumiza Tyson zaidi na badala yake alijitahidi kuwapa mashabiki burudani “Nampenda Mike,” alisema Paul baada ya pambano hilo.
Pia alieleza kuwa pambano hilo lilikuwa tofauti na mapambano yake ya awali, akisisitiza kwamba aliweza kubaini haraka kasi ya Tyson na kufanikisha mbinu zake “Nilimudu kumshinda kwa urahisi na nilifurahia pambano hilo,” alisema Paul huku akieleza kuwa yuko tayari kupambana na majina makubwa zaidi katika ndondi.
Licha ya matokeo hayo, Jake Paul, Mike Tyson, pamoja na mabondia Amanda Serrano na Katie Taylor, wamefungiwa kushiriki mapambano kwa muda wa siku 45 huku ikielezwa marufuku hiyo ni ya kawaida kwa Mabondia baada ya kushiriki pambano kubwa na imelenga kuwapa muda wa kupona.