Mbunge wa Iramba Mashariki Mhe. Francis Mtinga ametoa wito kwa vijana, wanawake na watu wenye ulevamavu wilayani Mkalama kutumia vizuri mikopo wanayopewa kwa kuwekeza katika biashara zenye tija ili waweze kujikwamua kiuchumia pamoja na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Wito huo ameutoa Februari 11,2025 wakati wa hafla ya utoaji mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana pamoja na Watu wenye Ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Sheketela wilayani hapa.
“Mikopo hii haina riba na pia mikopo hii si zawadi bali ni mtaji wa kubadili masiha yetu, hivyo twendeni tukasimamie vizuri biashara zetu ili tuweze kupata faida na kuweza kukuza uchumi wetu” Mhe. Mtinga
Aidha Mhe. Mtinga amevitaka vikundi hivyo kuhakikisha vinarejesha mikopo kwa wakati kulingana na taratibu zilizowekwa ili kutoa nafasi kwa watu wengine wenye sifa kunufaika na mikopo hiyo katika awamu nyingine
“niwasihi kuwa marejesho ni lazima, tufanye kazi na tukumbuke kurejesha kwa ajili ya wengine wanufaike pia” Mhe. Mtinga.
Awali akizungumza kuhusu mikopo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Asia Messos amesema mara baada ya dirisha kufunguliwa, jumla ya vikundi 143 vilituma maombi ambapo vikundi 73 vimefanikiwa kupata mikopo hiyo katika awamu ya kwanza. Vikundi hivyo, Wanawake 51, vijana 19 na Vikundi 3 vya Watu Wenye Ulemavu.
“Katika awamu ya kwanza tumetenga milioni 395.5 kwa ajili ya vikundi 73’’ DED Asia
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mikopo hiyo, Bi. Joyce Martini, mkazi wa kijiji cha Mazangili, kata ya Nkinto wilayani hapa ameishukuru serikali kwa kuwapatia mikopo hiyo kwani itawasaidia katika biashara yao ya ufungaji Ng’ombe na Kuku.
“Asante kwa Mama Samia kwa kutuona wananchi wa Mkalama hasa kina mama kwani mikopo hii itatuwezesha kuendesha biashara yetu ya ufugaji lakini pia niwakumbushe wanufaika wenzangu kurejesha mikopo hii kwa wakati” Bi. Joyce Martini