Misaada ya dawa, chakula na mahitaji mengine imeendelea kupelekwa katika eneo la mashariki mwa Libya baada ya eneo hilo kukumbwa na mafuriko makubwa.
Tume ya Msaada ya Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) imesema, mashirika tisa ya Umoja huo yanaendelea kupeleka misaada katika maeneo yaliyoathirika na kimbunga Daniel na mafuriko ya ghafla yaliyotokea siku chache zilizopita.
Umoja wa Mataifa umeomba dola za kimarekani milioni 71.4, kati yao dola milioni 10 zimetolewa katika Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Mataifa ili kuwasaidia watu walioathirika na mafuriko.
Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha nchini Libya kimeonya dhidi ya kutumia maji katika mji wa Derna ulioathiriwa zaidi na mafuriko hayo, ambayo yamechafuliwa na majitaka kwa hofu ya kuenea kwa magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa maji.