Leo September 17, 2018 Kufuatia matukio ya kukosekana kwa uaminifu kwa wanavikundi wanaowekeza pesa ili kujikwamua kiuchumi, benki ya CRDB imekuja na bidhaa tatu mpya kwa wateja wake ikiwamo wenye vikundi vya vikoba kupata akaunti kupitia simu zao za mkononi ili kuondokana na changamoto ambazo zinawakabili.
Meneja wa huduma za fedha kwa njia ya mtandao wa benki hiyo, Edith Metta, ameyasema hayo wakati akitoa elimu kwa waandishi wa habari kuhusiana na huduma hizo mpya kwa wateja.
Alizitaja huduma hizo kuwa ni akaunti ya kikundi, akaunti ya akiba na akaunti ya malipo.
Metta alisema kumekuwa na changamoto katika baadhi ya vikundi vya fedha ikiwamo vikoba za kupotea kwa fedha au mmoja kukimbia nazo hivyo wameamua kuja na suluhisho kwa vikundi ili fedha zao ziwe salama.
Alisema wanachama wanauwezo wa kufungua akaunti ya pamoja kupitia simu zao za mkononi na kisha kusajili jina la kikundi na kuanza kuweka fedha pamoja na kutoa bila kuwepo na makato.
“Mwanachama wa kikundi ana uwezo wa kuangalia kiasi cha salio kilichopo katika akaunti ya kikundi na endapo kuna fedha imetolewa kinyemela wanajua kwa wakati na kuepusha mwanachama kukimbia na fedha ama kuambiwa fedha imeibiwa,” alisema
Alisema akaunti ya kikundi ni nzuri kwani fedha zao zinakuwa salama na endapo kunakuwa na udanganyifu wanajua mapema na kuanza kuchukua hatua.
Pia alisema fedha za wanachama zinakuwa salama na hakutakuwa na matukio ya kuibiwa kwa fedha za kikundi kama ilivyo katika maeneo mengine kumekuwa na malalamiko ya kuibiwa fedha za vikoba ama kupotea.
Aidha, alisema kuwa akaunti inaanza kwa kikundi cha watu watatu hadi na 3,000 na kiwango cha mwisho cha kuweka fedha ni Milioni 50 kwa kila kikundi.
Alisema kwa kikundi ambacho kitakuwa vizuri katika uwekaji wa fedha huwafuatilia na baada ya muda wanaweza kuwapatia mkopo ili wajijenge vizuri kiuchumi.
Alisema kaunti hiyo sio kwa vikundi tu hata kwa vikao vya harusi wanaweza kujisajili na kufanya malipo kupitia akaunti ya kikundi na fedha zao zikawa salama kuliko kumuachia mweka hazina kwenda nazo nyumbani.
“Kuliko mtu aende benki kutoa fedha ya mchango ama mweka hazina kupata shida ya kuandaa taarifa ya fedha ni kwamba ukishaingia katika hiyo akaunti utakuwa unahamisha fedha na kuona salio bila kuandaa taarifa ya fedha,” alisema Metta.
Aidha, alisema ili mteja aweza kupata akaunti kupitia simu yake ya mkononi atatakiwa kubonyeza *150*62 na kufuata maelezo ambapo atajisajili kupitia kitambusho cha kura ama cha utaifa na akaunti kuipata ndani ya dakika mbili.
Metta alisema lengo la huduma hiyo ni kuwafikia wateja wake hususani katika maeneo ya vijijini ambao wamekuwa wakihifadhi fedha zao katika mfumo usio rasmi jambo ambalo wanahatarisha usalama wa fedha zao.