Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la reli nchini (TRC) Masanja Kadogosa ametembelea majeruhi wa ajali ya treni mkoani Kigoma na kutangaza kuwa serikali itagharamia matibabu ya abiria 73 waliojeruhiwa katika ajali ya treni ya abiria iliyoanguka eneo la Lugufu wilaya ya Uvinza usiku wa kuamkia Agosti 28 mwaka huu.
Kadogosa amesema hayo alipowatembelea majeruhi katika hospitali ya rufaa ya mkoa kigoma Maweni na hospitali ya wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ambapo amesema kuwa pamoja na kugharamia matibabu kwa majeruhi wote pia TRC itawasafirisha majeruhi wote wa ajali hiyo kuendelea na safari zao hadi wanapokwenda.
Akiwa hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk.Lameck Mdengo amesema kuwa hadi sasa wamebaki wagonjwa wanne kati ya watano waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya Uvinza, Dk.David Patrick George amesema kuwa wagonjwa 73 walipokewa hospitalini hapo siku ya ajali na hadi kufikia leo mchana wakati Mkurugenzi Mkuu anatembelea majeruhi hospitalini hapo walibaki wagonjwa sita ambapo katika wagonjwa hao watatu waliomba kuendelea na safari baada ya ziara ya Mkurugenzi Mkuu hospitalini hapo na wagonjwa watatu watahamishiwa hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni kwa matibabu zaidi.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali za rufaa mkoa Kigoma akiwemo Hamida Hamza ambaye ameumia mgongo na mbavu amelishukuru shirika la reli, uongozi wa serikali ya mkoa na waganga katika hospitali za Uvinza na kwa jitihada kubwa walizofanya tangu ajali ilipotokea hadi sasa wanapoendelea na matibabu ambapo hawajadaiwa gharama zozote za matibabu wala chakula.
Hadi sasa hakuna kifo kilichoripotiwa ambapo Kwa majeruhiwa wanne waliopo Hospitali ya Rufaa Maweni wanaendelea na matibabu na vipimo kutazama hali zao zaidi.