Mkurugenzi wa Huduma ya Secret Service, aliyekosolewa kutokana na jaribio la mauaji dhidi ya Donald Trump mnamo Julai 13, amejiuzulu, vyombo vya habari kadhaa vya Marekani vimeripoti.
Kimberly Cheatle, mkuu wa Huduma Secret Service inayohusika na ulinzi wa watu wa ngazi za juu wa Marekani, alitambua kutofaulu na alipigiwa simu nyingi za kujiuzulu.
Cheatle alikuwa akikabiliwa na shinikizo kutoka kwa viongozi wa vyama viwili vikubwa nchini humo ajiuzulu baada ya mtu mwenye bunduki, mwenye umri wa miaka 20 kumjeruhi Trump mgombea wa sasa wa urais kwa tiketi ya chama cha Republican katika mkutano wa kampeni wa Julai 13 mjini Butler, Pennsylvania.
Cheatle alifika mbele ya kamati ya bunge siku ya Jumatatu na kusema kuwa shambulizi dhidi ya Trump, ambaye alijeruhiwa kidogo kwenye sikio lake la kulia, lilikuwa kushindwa kwa idara hiyo ya Secret Service.
Wabunge walimhoji Cheatle kuhusu maandalizi ya usalama kabla ya mkutano wa kampeni wakati wa kikao cha saa sita cha Kamati ya Uangalizi ya Bunge.
Warepublican na Wademokrat walimtaka Cheatle ajiuzulu.