Waendesha mashtaka nchini Korea Kusini wamemfungulia mashtaka Waziri wa zamani wa Ulinzi Kim Yong-hyun kwa kuhusika kwake katika tamko lililodumu kwa muda mfupi la Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol la sheria ya kijeshi. Anashtakiwa kwa uasi na matumizi mabaya ya mamlaka.
Yoon alitekeleza hatua hiyo Desemba 3, lakini wabunge walibatilisha uamuzi huo bungeni saa chache baadaye.
Waendesha mashtaka walisema jana Ijumaa kwamba Kim aliamuru wanajeshi kuwazuia wabunge kuingia katika Bunge la Kitaifa.
Pia wanamtuhumu kwa kuamuru wanajeshi kuwaweka kizuizini maafisa akiwemo kiongozi wa chama tawala cha People Power wakati huo, na mkuu wa chama kikuu cha upinzani.
Waendesha mashtaka wanasema Kim aliamuru wanajeshi kuchukua udhibiti wa Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi.
Wanasema Yoon, Kim na maafisa wengine walijadili sheria ya kijeshi mara nyingi tangu mwezi Machi. Wanasema Kim alihusika katika maandalizi hayo, na aliandika maandishi yatakayosomwa na Yoon.