Jack Teixeira, mjumbe wa Walinzi wa Kitaifa wa Wanahewa wa Marekani ambaye alitoa siri na hati za Pentagon mwaka jana katika moja ya ukiukaji mkubwa wa sheria na wa kijasusi amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.
Teixeira, mwenye umri wa miaka 22, alikiri hatia mwezi Machi kwa kuhifadhi na kusambaza taarifa za ulinzi wa taifa kimakusudi.
Akiwa katika kituo cha Walinzi wa Kitaifa wa wana hewa, alipata nyenzo kama vile ramani, picha za setilaiti, na taarifa za kijasusi kwa washirika wa Marekani, ambazo kisha alishiriki kwenye jukwaa la mtandaoni maarufu kwa wachezaji. Miongoni mwa hati zilizovuja ni habari nyeti kuhusu vita vya Ukraine.
Waendesha mashtaka walikuwa wamemsihi Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani, Indira Talwani kutoa kifungo cha miaka 16 na nusu, wakati utetezi wa Teixeira ulitaka kifungo cha miaka 11.
Katika kutetea adhabu ya kupunguzwa, mawakili wake walitaja uzoefu wake wa uonevu wakati wa shule ya upili na ndani ya kitengo chake cha kijeshi, pamoja na mapambano yake ya kutengwa.
Kinyume chake, waendesha mashtaka walidai kwamba hukumu kali zaidi ilihitajika, ikionyesha kesi hiyo kuwa mojawapo ya ukiukaji mkubwa wa Sheria ya Ujasusi katika historia ya Marekani.
Walidai kwamba Teixeira alikuwa anajua hatari kwa nchi yake lakini alichagua kuendelea bila kujali.