Watu wasiopungua wanane wamefariki dunia katika mripuko uliotokea katika kiwanda kimoja cha kuhifadhi na kusambaza mafuta huko Conakry, mji mkuu wa Guinea.
Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo leo Jumatatu na kuongeza kuwa, watu wengine 84 wamejeruhiwa katika mripuko huo uliotokea usiku wa kuamkia leo, na tayari wamefikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Afisa mwandamizi wa polisi amenukuliwa na shirika la habari la al-Jazeera akisema kuwa, yumkini idadi ya wahanga wa mkasa huo ikaongezeka kutokana na hali mbaya ya majeruhi.
Habari zaidi zinasema kuwa, mamia ya wakazi wa wilaya ya Kaloum, viungani mwa Conakry wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na kuenea kwa kasi moto uliosababishwa na mripuko huo. Nyumba na majengo kadhaa yameteketea kwa moto na kugeuka majivu.