Mlipuko mkubwa ulisababisha moto katika kiwanda cha kutengeneza dawa kusini mwa India, na kuua wafanyakazi wasiopungua 15, polisi walisema Alhamisi.
Zaidi ya watu 40 walijeruhiwa katika mlipuko huo na moto katika kinu cha kemikali cha kiwanda hicho katika jimbo la Andhra Pradesh Jumatano na wamelazwa hospitalini, afisa wa polisi M. Deepika alisema, akiongeza kuwa baadhi yao walikuwa katika hali mbaya.
Shirika la habari la Press Trust of India liliripoti matukio ya kuhuzunisha huku ngozi za wafanyakazi kadhaa zikichubuka. Magari ya wagonjwa yaliwasafirisha hadi hospitali.
Maafisa wanashuku sababu ilihusiana na umeme katika kiwanda hicho. Mamlaka za serikali zimeamuru uchunguzi ufanyike.
Mlipuko huo ulitokea katika Kampuni ya Escientia wilayani Anakapalle. Kiwanda hicho kiko takriban kilomita 350 (maili 220) kaskazini mashariki mwa Amaravati, mji mkuu wa Andhra Pradesh.
Kampuni hiyo yenye umri wa miaka 5 hutengeneza kemikali za kati na viambato vya kazi vya dawa.
Habari za mlipuko huo zilipoenea, mamia ya wanafamilia na watu wa ukoo wa wafanyakazi walikimbilia kwenye kiwanda hicho ili kujua kilichowapata wapendwa wao.
Takriban wafanyikazi 380 hufanya kazi zamu mbili kwenye kiwanda. Wafanyakazi wengi walitoroka kwa sababu walikuwa kwenye mapumziko ya chakula cha mchana wakati mlipuko ulipoanzisha moto.