Kampuni ya Meta chini ya uongozi wa Mark Zuckerberg imetoa dola milioni 1 (takriban shilingi bilioni 2.5 za Kitanzania) kusaidia mfuko wa uapisho wa Rais mteule wa Marekani Donald Trump ambapo mchango huu unakuja baada ya msimu wa uchaguzi uliojaa mvutano ambapo Trump aliwahi kumtishia Zuckerberg na kusema anapaswa kufungwa Gerezani maisha ikiwa angeingilia uchaguzi wa mwaka 2024.
Kwa miaka kadhaa uhusiano kati ya Zuckerberg na Trump umekuwa na mabadiliko makubwa mara nyingine wakikosoana na mara nyingine wakishirikiana na Zuckerberg amewahi kukosoa sera za uhamiaji za Trump mwaka 2017 huku Facebook pia ikisimamisha akaunti ya Trump baada ya vurugu za Januari 6 mwaka 2021, hata hivyo hatua hii ya sasa inaonekana kama juhudi za Zuckerberg kurekebisha uhusiano na upande wa Republican.
Taarifa zinaeleza kuwa Meta haikutoa mchango wowote kwa mfuko wa uapisho wa Trump mwaka 2017 wala kwa Joe Biden mwaka 2021 lakini miaka ya karibuni Zuckerberg ameonekana kujaribu kujenga Daraja na Viongozi wa Republican kwa kuandaa mikutano na vikao ambapo Katika mojawapo ya mikutano hiyo Zuckerberg alionyesha teknolojia ya miwani ya Meta aina ya Ray-Ban na kumpa Trump zawadi ya jozi moja.
Aidha mchango wake huu umeelezwa kuwa ulikuwa umeamuliwa kabla ya mkutano huo na unalenga kuonyesha kuwa Meta haina upande maalum katika masuala ya kisiasa na juhudi hizi za Zuckerberg ni kupunguza lawama za upendeleo wa kisiasa zilizokuwa zikielekezwa kwake hasa baada ya uchaguzi wa 2020 ambapo alitoa dola milioni 400( takriban trilion 1 za kitanzania) kusaidia miundombinu ya uchaguzi hatua ambayo ilikosolewa na baadhi ya Wajumbe wa Republican.