Raia wa Rwanda Denis Kazungu amekiri kosa la kuua watu 14 wengi wao wakiwa wanawake na kuficha miili yao ndani ya nyumba yake mjini Kigali.
Kazungu, mwenye umri wa miaka 34 alikiri kuwa na hatia katika mashtaka aliyosomewa ambayo ni pamoja na mauaji, ubakaji na wizi. Alifikishwa katika Mahakama ya Kicukiro katika mji mkuu huo wa Rwanda jana Alkhamisi.
Mshtakiwa huyo alitabasamu huku polisi wakimwingiza ndani ya chumba cha mahakama, lakini hakuonekana kuonyesha hisia zozote wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake.
Polisi waligundua maiti 12 nyumbani kwake lakini mshtakiwa mwenyewe amesema aliua watu wengine wawili ambao miili yao haijapatikana.
Kwa mujibu wa mamlaka husika za Rwanda, waliouliwa na Kazungu ni pamoja na wanawake 11 na mwanamume mmoja; hata hivyo jinsia za watu wengine wawili ambao mshtakiwa huyo amesema aliwaua hazijaweza kufahamika mara moja.