Morocco, nchi ambayo kilimo ni sekta muhimu, inaelekea kwa mwaka wake wa sita mfululizo wa ukame kutokana na kupungua kwa mvua katika miezi ya hivi karibuni inayohusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, Waziri wa Vifaa na Maji wa Morocco, Nizar Baraka, alisema Alhamisi.
“Tumeingia katika hatua mbaya baada ya miaka mitano mfululizo ya ukame ambayo nchi yetu haijawahi kukumbana nayo hapo awali,” alisema Bw. Baraka katika mkutano na wanahabari.
Mvua imeshuka kwa asilimia 67 katika miezi ya hivi karibuni ikilinganishwa na mwaka unaochukuliwa kuwa wa kawaida, na “miezi mitatu iliyopita (kuanzia Oktoba hadi Desemba) inaonyesha kuwa tunaelekea mwaka mwingine wa ukame”, aliongeza waziri huyo.
Nchini Morocco, kilimo kinaajiri theluthi moja ya watu wenye umri wa kufanya kazi na kinachangia 14% ya mauzo ya nje ya nchi.
Mkazo wa maji nchini Morocco umechochewa na kuongezeka kwa joto, jambo ambalo limeongeza uvukizi wa maji kutoka kwenye mabwawa. Wizara ya Kilimo inatabiri ongezeko la wastani la joto la nyuzi joto 1.3 kufikia 2050.