Maofisa wa jeshi la maji nchini Morocco wamewaokoa wahamiaji 141 wa Afrika kutoka kwenye boti walimokuwa wakisafiria iliokumbwa na changamoto wakati wakielekea katika visiwa Canary nchini Uhispania wakitokea nchini Mauritania.
Shughuli ya kuwaokoa wahamiaji hao imefanyika hapo jana Jumapili kilomita 274 Kusini Magharibi mwa mji wa Dakhla-Magharibi mwa jangwa la Sahara.
Kwa mujibu wa uongozi wa jeshi la maji la Morocco, wahamiaji hao waliondoka pwani ya Mauritania tarehe 10 ya mwezi Februari.
Mwaka uliopita, visiwa vya Canary viliripotiwa kuwapokea karibia wahamiaji elfu 32, idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa tangu mwaka wa 2006.
Mwezi Januari, mamlaka nchini Uhispania iliripoti kuendelea kuandikisha idadi kubwa ya wahamiaji wanaowasili katika visiwa hivyo, sehemu kubwa ya boti za wahamiaji zikitokea nchini Mauritania.
Idadi kubwa ya wahamiaji wamekuwa wakiripotiwa kuzama wakijaribu kuvuka kwenda bara Ulaya kutoka bara Afrika wakitumia njia hatari zikiwemo boti za mbao.