Mtayarishaji maarufu wa maudhui ya YouTube Jimmy Donaldson maarufu kama MrBeast ameibua gumzo baada ya kutangaza nia ya kuinunua TikTok iwapo itapigwa marufuku Nchini Marekani na hii ni kutokana na TikTok kukabiliwa na tishio la kufungwa kwa huduma zake kwa Watumiaji wa Marekani ifikapo Januari 19, 2025 endapo Mahakama haitasitisha marufuku hiyo.
Kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa X, MrBeast aliandika “Sawa, nitanunua TikTok ili isipigwe marufuku.” Kisha baadaye aliongeza kuwa Mabilionea kadhaa wamejitokeza na kumshawishi kushirikiana nao katika kufanikisha mpango huo ingawa bado haijabainika wazi kama alikuwa akimaanisha kwa dhati au ni sehemu ya utani wake wa kawaida.
Aidha kupitia Sheria iliyosainiwa na Rais Joe Biden mwaka 2024 inaitaka kampuni ya ByteDance kutoka China ambayo ndio kampuni mama ya TikTok kuuza shughuli zake za Marekani ili kuepusha marufuku hiyo ambapo Serikali ya Marekani inadai kuwa TikTok inahatarisha usalama wa Taifa kwa kuruhusu China kukusanya data za Watumiaji wake madai ambayo kampuni ya ByteDance imekanusha mara kadhaa.
Endapo marufuku hiyo itatekelezwa itafanya Watumiaji wa TikTok Nchini Marekani kutoweza kupakua Programu hiyo tena huku waliopo hivi sasa wakiendelea kuitumia kwa muda mfupi kabla ya kufungwa rasmi.
TikTok bado haijatoa tamko rasmi kuhusu hali hii lakini mpango wa MrBeast umeleta matumaini kwa baadhi ya Watumiaji wa Marekani huku wengine wakisubiri kuona kama nia yake itageuka kuwa hatua halisi ya kibiashara.